Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 3 ya Kwaresima (Jumapili, Machi 20, 2022)  

Somo la 1

Kut 3:1-8a, 13-15

Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu. Malaika wa Bwana akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea. Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei. Bwana alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa. Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu. Tena akasema, Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu. Bwana akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; Musa akamwambia Mungu, Tazama, nitakapofika kwa wana wa Israeli, na kuwaambia, Mungu wa baba zenu amenituma kwenu; nao wakaniuliza, Jina lake n'nani? Niwaambie nini? Mungu akamwambia Musa, MIMI NIKO AMBAYE NIKO;akasema,Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli;MIMI NIKO amenituma kwenu. Tena Mungu akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli maneno haya, Bwana, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu; hili ndilo jina langu hata milele, nalo ni kumbukumbu langu hata vizazi vyote.

Wimbo wa Katikati

Zab 103:1-4, 6-8, 11

(K) Bwana amejaa huruma na neema.

Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Naam, vyote vilivyo ndani yangu
Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote.
(K) Bwana amejaa huruma na neema.

Akusamehe maovu yako yote,
Akuponya magonjwa yako yote,
Aukomboa uhai wako na kaburi,
Akutia taji ya fadhili na rehema,
(K) Bwana amejaa huruma na neema.

Bwana ndiye afanyaye mambo ya haki,
Na hukumu kwa wote wanaoonewa.
Alimjulisha Musa njia zake,
Wana wa Israeli matendo yake.
(K) Bwana amejaa huruma na neema.

Bwana amejaa huruma na neema,
Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,
Kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao.
(K) Bwana amejaa huruma na neema.

Somo la 2

1Kor 10:1-6, 10-12

Ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari; wote wakala chakula kile kile cha roho; wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. Lakini wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani. Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani. Wala msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika, wakaharibiwa na mharabu. Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.

Shangilio

Zab 95:8

Msifanye migumu mioyo yenu;
Lakini msikie sauti yake Bwana.

Injili

Lk 13:1-9

Wakati ule walikuwapo watu waliompasha Yesu habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao. Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate. Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu? Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate.

Maoni


Ingia utoe maoni