Masomo ya Misa
Ubatizo wa Bwana (Jumapili, Januari 09, 2022)
Isa 42:1-4,6-7
Bwana asema: Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu. Hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njia kuu. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli. Hatazimia, wala hatakata tamaa, hata atakapoweka hukumu duniani; na visiwa vitaingojea sheria yake. Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa; kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa.
Zab 29:1-4, 9-10
Mpeni Bwana, enyi wana wa Mungu,
Mpeni Bwana utukufu na nguvu;
Mpeni Bwana utukufu wa jina lake;
Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu.
(K) Bwana atawabariki watu wake kwa amani.
Sauti ya Bwana i juu ya maji;
Mungu wa utukufu alipiga radi;
Bwana yu juu ya maji mengi.
Sauti ya Bwana ina nguvu;
Sauti ya Bwana ina adhama;
(K) Bwana atawabariki watu wake kwa amani.
Sauti ya Bwana yawazalisha ayala,
Na ndani ya hekalu lake Wanasema wote, Utukufu.
Bwana aliketi juu ya Gharika; Naam,
Bwana ameketi hali ya mfalme milele.
(K) Bwana atawabariki watu wake kwa amani.
Mdo 10:34-38
Siku ile: Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye. Neno lile alilowapelekea wana wa Israeli akihubiri habari njema ya amani kwa Yesu Kristo (ndiye Bwana wa wote), jambo lile ninyi mmelijua, lililoenea katika Uyahudi wote likianzia Galilaya, baada ya ubatizo aliouhubiri Yohana; habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.
Mk 9:7
Aleluya, aleluya
Mbingu zilifunguka na sauti ya Baba ikasikika "Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu msikieni yeye."
Aleluya.
Lk 3:15-16, 21-22
Siku ile: Watu walipokuwa wakingoja yatakayotokea, wote wakiwaza-waza mioyoni mwao habari za Yohana, kama labda yeye ndiye Kristo, Yohana alijibu akawaambia wote, Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini yuaja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto; Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka; Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.
Maoni
Hancy Sunday
AminaJoshua Lonyakol
AminaMarygoreth Baijukya
Sifa kwako ee Kristo, AminaIngia utoe maoni