Masomo ya Misa
Jumanne ya 33 ya Mwaka (Jumanne, Novemba 16, 2021)
2Mak 6:18-31
Eliazari, mmoja wa waandishi wakuu, mkuu wa umri mkubwa na sura njema, alishurutishwa kufunua kinywa chake kulishwa nyama ya nguruwe. Lakini akaitema ile nyama, akasogea mwenyewe kwenye mahali pa kuteswa, akiona afadhali kufa kwa heshima kuliko kwa unajisi. Akatenda kama yampasavyo mtu aliyekaza nia yake kuvikataa vitu visivyo halali kuonjwa hata kwa kutaka kujiokoa maisha. Basi, wale waliosimamia dhabihu hiyo haramu, kwa kuwa wamejuana naye kwa miaka mingi walimchukua kando wakamsihi alete nyama yake mwenyewe, iliyo halali ya kuliwa, na kufanya kana kwamba anaila nyama ya dhabihu, kama mfalme alivyoamuru. Hivyo atajiponya na mauti, na kutendewa nao kwa hisani kwa sababu ya urafiki wao wa tangu zamani. Lakini yeye aliikaza nia yake madhubuti, nia iliyostahili umri wake na jadi yake, na mvi zake stahivu, na mwendo wake wa adili tangu utoto wake katika kuzishika amri takatifu zilizotolewa na Mungu. Akakataa kabisa, na kuwaambia wampeleke kuzimuni upesi akisema haipatani na miaka yetu kudanganya, isije vijana wengi wadhani ya kuwa Eliazari, katika mwaka wake wa tisini, ameicha dini yake kwa dini ya kigeni; na hivyo, kwa sababu ya udanganyifu wangu, watapotoshwa na mimi mwenyewe nitajipatia unajisi na aibu katika uzee wangu. Na hata nikiepukana na adhabu ya wanadamu sasa, lakini sitaweza kuepukana na mikono ya Mwenyezi, nikiwa hai au nimekufa. Basi, nikitoa maisha yangu sasa kwa ushujaa, nitajionyesha kuwa nimestahili miaka yangu mingi, na kuwaachia vijana mfano wa kufa mauti ya fahari kwa hiari na kwa uthabiti, kwa ajili ya amri takatifu zenye heshima. Alipokwisha kusema hayo, alipaendea mara mahali pa kuteswa. Nao waliokuwa wakimwonyesha urafiki walibadili nia zako kwa wabaya kwa sababu ya maneno yake waliyoyaona ya kiwazimu. Naye alipokuwa kufani kwa ajili ya mapigo yake, aliugua akasema, kwake Bwana ajuaye yote ni dhaniri ya kuwa, ingawa ningaliweza kuepukana na mauti, lakini ninavumilia maumivu makali mwlini mwangu; hata rohoni mwangu ninayavumilia kwa furaha kwa sababu ya kicho changu kwake. Hivyo alikufa; na kwa kufa kwake aliacha mfano wa unyofu na ukumbusho wa wema, si kwa vijana tu, ila kwa jamii yote ya taifa lake.
Zab 3:1-6
Bwana, watesi wangu wamezidi kuwa wengi,
Ni wengi wanaonishambulia,
Ni wengi wanaoiambia nafsi yangu,
Hana wokovu huyu kwa Mungu.
(K) Bwana ananitegemeza.
Na Wewe, Bwana, U ngao yangu pande zote,
Utukufu wangu na mwinua kichwa changu.
Kwa sauti yangu namwita Bwana
Naye aniitikia toka mlima wake mtakatifu.
(K) Bwana ananitegemeza.
Nalijilaza nikalala usingizi, nikaamka,
Kwa kuwa Bwana ananitegemeza.
Sitayaogopa makumi elfu ya watu,
Waliojipanga juu yangu pande zote.
(K) Bwana ananitegemeza.
Lk 19:1-10
Yesu alipoingia Yeriko alipita katikati yake. Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri. Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo. Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile. Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako. Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha. Hata watu walipoona, walinung'unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi. Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne. Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.
Maoni
Betram Mushi
Milele....Amina...Tumshukuru..Mungu.Ingia utoe maoni