Jumanne. 26 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 22 ya Mwaka (Jumapili, Agosti 29, 2021)  

Somo la 1

Kum 4:1-2, 6-8

Na sasa, Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu. Msiliongeze neno niwaamurulo wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za Bwana, Mungu wenu, niwaamuruzo. Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili. Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama Bwana, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo.

Wimbo wa Katikati

Zab 15:1-5

Bwana, ni nani atakayefanya maskani yake
Katika kilima chako kitakatifu?
Ni mtu aendaye kwa ukamilifu?
Ni mtu aendaye kwa ukamilifu,
Na kutenda haki;
Asemaye kweli kwa moyo wake.
(K) Bwana, ni nani atakayekaa katika hema yako?

Ni yeye ambaye hakumtenda mwenziwe mabaya,
Wala hakumsengenya jirani yake.
Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa,
Bali huwaheshimu wamchao Bwana.
(K) Bwana, ni nani atakayekaa katika hema yako?

Ni yeye ambaye hayabadili maneno yake,
Ingawa ameapa kwa hasara yake.
Ambaye hakutoa fedha yake apate kula riba,
Wala hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia.
Mtu atendaye mambo hayo hataondoshwa milele.
(K) Bwana, ni nani atakayekaa katika hema yako?

Somo la 2

Yak 1:17-18, 21-22, 27

Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeukageuka. Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake. Kwa hiyo wekeeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu. Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii. Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa.

Shangilio

Yn 6:63, 68

Aleluya, aleluya.
Bwana, maneno yako ni roho, tena ni uzima, Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya.

Injili

Mk 7:1-8, 14-15, 21-23

Mafarisayo, na baadhi ya waandishi waliotoka Yerusalemu, wakakusanyika mbele ya Yesu wakaona wengine katika wanafunzi wake wakila vyakula kwa mikono najisi, yaani, isiyonawiwa. Kwa maana Mafarisayo na Wayahudi wote wasiponawa mikono mpaka kiwiko, hawali, wakishika mapokeo ya wazee wao; tena wakitoka sokoni, wasipotawadha, hawali; na yako mambo mengine waliyopokea huyashika, kama kuosha vikombe, na midumu, na vyombo vya shaba. Basi wale Mafarisayo na waandishi wakamwuliza, Mbona wanafunzi wako hawaendi kwa kuyafuata mapokeo ya wazee, bali hula chakula kwa mikono najisi? Akawaambia, Isaya alitabiri vema juu yenu ninyi wanafiki, kama ilivyoandikwa, Watu hawa huniheshimu kwa midomo Ila mioyo yao iko mbali nami; Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu. Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu. Akawaita makutano tena, akawaambia, Nisikieni nyote na kufahamu. Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu. Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi.

Maoni

Martha John

Good

Martha John

Good

Ingia utoe maoni