Masomo ya Misa
Jumatano ya 3 ya Mwaka (Jumatano, Januari 27, 2021)
Ebr 10:11-18
Kila kuhani husimama kila siku akifanya ibada, na kutoa dhabihu zile zile mara nyingi; ambazo haziwezi kabisa kuondoa dhambi. Lakini huyu, alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi mkono wa kuume wa Mungu; tangu hapo akingojea hata adui zake wawekwe kuwa chini ya miguu yake. Maana kwa toleo moja amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa. Na Roho Mtakatifu naye amshuhudia; kwa maana, baada ya kusema, Hili ni agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana, Nitatia sheria zangu mioyoni mwao, Na katika nia zao nitaziandika; ndipo anenapo, Dhambi zao na uasi wao sitaukumbuka tena kabisa. Basi, ondoleo la hayo likiwapo, hapana toleo tena kwa ajili ya dhambi.
Zab 110:1-4
Neno la Bwana kwa Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume,
Hata niwafanyapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako.
(K) Wewe ndiwe kuhani hata milele kwa mfano wa Melkizedeki.
Bwana atainyosha toka Sayuni Fimbo ya nguvu zako.
Uwe na enzi kati ya adui zako;
(K) Wewe ndiwe kuhani hata milele kwa mfano wa Melkizedeki.
Watu wako wanajitoa kwa hiari, Siku ya uwezo wako;
Kwa uzuri wa utakatifu,
Tokea tumbo la asubuhi, Unao umande wa ujana wako.
(K) Wewe ndiwe kuhani hata milele kwa mfano wa Melkizedeki.
Bwana ameapa, Wala hataghairi,
Ndiwe kuhani hata milele,
Kwa mfano wa Melkizedeki.
(K) Wewe ndiwe kuhani hata milele kwa mfano wa Melkizedeki.
Mk 4:1-20
Yesu alianza kufundisha tena kando ya bahari. Wakamkusanyikia mkutano mkubwa mno, hata yeye akapanda chomboni, akakaa baharini, mkutano wote ulikuwako juu ya nchi kavu kando ya bahari. Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, akawaambia katika mafundisho yake, Sikilizeni; Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda; ikawa alipokuwa akipanda, mbegu nyingine ilianguka kando ya njia, wakaja ndege wakaila. Nyingine ikaanguka penye mwamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara ikaota kwa kuwa na udongo haba; hata jua lilipozuka iliungua, na kwa kuwa haina mizizi ikanyauka. Nyingine ikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea ikaisonga, isizae matunda. Nyingine zikaanguka penye udongo ulio mzuri, zikazaa matunda, zikimea na kukua, na kuzaa, moja thelathini, moja sitini, na moja mia. Akasema, Aliye na masikio ya kusikilia, na asikie. Naye alipokuwa peke yake, wale watu waliomzunguka, na wale Thenashara, walimwuliza habari za ile mifano. Akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuijua siri ya ufalme wa Mungu, bali kwa wale walio nje yote hufanywa kwa mifano, ili wakitazama watazame, wasione; Na wakisikia wasikie, wasielewe; Wasije wakaongoka, na kusamehewa. Akawaambia, Hamjui mfano huu? Basi mifano yote mtaitambuaje? Mpanzi huyo hulipanda neno. Hawa ndio walio kando ya njia lipandwapo neno; nao, wakiisha kusikia, mara huja Shetani, akaliondoa lile neno lililopandwa mioyoni mwao. Kadhalika na hawa ndio wapandwao penye miamba, ambao kwamba wakiisha kulisikia lile neno, mara hulipokea kwa furaha; ila hawana mizizi ndani yao, bali hudumu muda mchache; kisha ikitokea dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara hujikwaa. Na hawa ndio wale wapandwao penye miiba; ni watu walisikiao lile neno, na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali, na tamaa za mambo mengine zikiingia, hulisonga lile neno, likawa halizai. Na hawa ndio waliopandwa penye udongo ulio mzuri; ni watu walisikiao lile neno na kulipokea, na kuzaa matunda, mmoja thelathini, mmoja sitini, na mmoja mia.
Maoni
Ingia utoe maoni