Masomo ya Misa
Jumatatu ya 23 ya Mwaka (Jumatatu, Septemba 07, 2020)
1Kor 5:1–8
Habari imeenea ya kuwa kwenu kuna zinaa, na zinaa ya namna isiyokuwako hata katika Mataifa, kwamba mtu awe na mke wa babaye. Nanyi mwajivuna, wala hamkusikitika, ili kwamba aondolewe miongoni mwenu huyo aliyetenda jambo hilo. Kwa maana kweli, nisipokuwapo kwa mwili, lakini nikiwapo kwa roho, mimi mwenyewe, nimekwisha kumhukumu yeye aliyetenda jambo hilo, kana kwamba nikiwapo. Katika jina la Bwana wetu Yesu, ninyi mkiwa mmekusanyika pamoja na roho yangu, pamoja na uweza wa Bwana wetu Yesu; kumtolea Shetani mtu huyo, ili mwili uadhibiwe, ili na roho iokolewe katika siku ya Bwana Yesu. Kujisifu kwenu si kuzuri. Hamjui kwamba chachu kidogo hulichachusha donge zima? Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo; basin a tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli.
Zab 5:4–6, 11
Unawachukia wote watendao ubatili.
Utawaharibu wasemao uongo;
Bwana humzira mwuaji na mwenye hila.
(K) Bwana, uniongoze kwa haki yako.
Maana huwi Mungu apendezwaye na ubaya;
Mtu mwovu hatakaa kwako;
Wajivunao hawatasimama mbele za macho yako.
(K) Bwana, uniongoze kwa haki yako.
Nao wote wanaokukimbilia watafurahi;
Watapiga daima kelele za furaha.
Kwa kuwa Wewe unawahifadhi,
Walipendao jina lako watakufurahia.
(K) Bwana, uniongoze kwa haki yako.
Zab 19:8
Aleluya, aleluya,
Amri ya Bwana ni safi, huyatia macho nuru.
Alelluya.
Lk 6:6–1
Ilikuwa siku ya sabato nyingine Yesu aliingia katika sinagogi akafundisha; na mlikuwamo mtu ambaye mkono wake wa kuume umepooza. Na waandishi na Mafarisayo walikuwa wakimvizia, ili waone kwamba ataponya siku ya sabato; kusudi wapate neno la kumshitakia. Lakini yeye atakayatambua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, Ondoka, simama katikati; akaondoka akasimama. Ndipo Yesu akawaambia, Nawauliza ninyi, Je! Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya; kuponya roho au kuangamiza? Akawakazia macho wote pande zote, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena. Wakajawa na uchungu, wakashauriana wao kwa wao wamtendeje Yesu.
Maoni
Ingia utoe maoni