Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 9 ya Mwaka (Jumamosi, Juni 06, 2020)  

Somo la 1

2 Tim 4:1-8

Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu walio hai na waliokufa; kwa kufunuliwa kwake na kwa ufalme wake; lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho. Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo. Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiliza huduma yako. Kwa maana, mimi sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika. Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake.

Wimbo wa Katikati

Tob 13:2, 6

Hurudi, na kurehemu tena,
Hushusha hata kuzimu, na kuinua tena;
Wala hakuna awezaye kujiepusha na mkono wake.
(K) Amehimidiwa Mungu aishiye milele.

Mkimgeukia kwa moyo wote na roho yote,
Na kutenda kweli zake.
Ndipo atakapowageukia ninyi,
Wala hatawaficheni uso wake.
(K) Amehimidiwa Mungu aishiye milele.

Angalieni atakavyowatendea:
Mshukuruni kwa vinywa vyenu vyote;
Mhimidini Bwana mwenye haki;
Mtukuzeni Mfalme wa milele.
(K) Amehimidiwa Mungu aishiye milele.

Katika nchi ya kufungwa kwangu namshukuru;
Nawahubiri taifa la wakosaji nguvu zake na enzi yake.
(K) Amehimidiwa Mungu aishiye milele.

Enyi wakosaji, geukeni, mkatende haki mbele zake;
Nani ajuaye kama atawakubali na kuwarehemu?
(K) Amehimidiwa Mungu aishiye milele.

Shangilio

Yn 10: 27

Aleluya, aleluya.
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya.

Injili

Mk 12:38-44

Yesu aliwaambia katika mafundisho yake: Jihadharini na waandishi, wapendao kutembea wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele katika karamu; ambao hula nyumba za wajane, na kwa unafiki husali sala ndefu; hawa watapata hukumu iliyo kubwa. Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi. Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa. Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.

Maoni

Joseph Pamba

Mbarikiwe sana.

Ingia utoe maoni