Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 12 ya Mwaka, Sherehe ya kuzaliwa Mt. Yoh (Ijumaa, Juni 24, 2016)  

Somo la 1

Isa 49:1-6

Nisikilizeni, enyi visiwa; tegeni masikio yenu, enyi kabila za watu mlio mbali sana; Bwana ameniita tangu tumboni; toka tumbo la mama yangu amenitaja jina langu. Naye anifanya kinywa changu kuwa kama upanga mkali; katika kivuli cha mkono wake amenisitiri; naye amenifanya kuwa mshale uliosuguliwa; katika podo lake amenificha; akaniambia; Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa. Lakini nikasema, Nimejitaabisha bure, nimetumia nguvu zangu bure bila faida; lakini hakika hukumu yangu ina Bwana, na thawabu yangu ina Mungu wangu. Na sasa Bwana asema hivi, yeye aliyeniumba tangu tumboni niwe mtumishi wake, ili nimletee Yakobo tena, na Israeli wakusanyike mbele zake tena; (maana mimi nimepata heshima mbele ya macho ya Bwana, na Mungu wangu amekuwa nguvu zangu); naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia.

Wimbo wa Katikati

Zab 139:1-3, 13-15

Ee Bwana, umenichunguza na kunijua.
Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu;
Umelifahamu wazo langu tokea mbali.
Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu,
Umeelewa na njia zangu zote.
(K)Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa.

Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu,
Uliniunga tumboni mwa mama yangu.
Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha.
Matendo yako ni ya ajabu,
(K)Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa.

Na nafsi yangu yajua sana,
Mifupa yangu haikusitirika kwako,
Nilipoumbwa kwa siri, Nilipoungwa kwa ustadi pande za chini za nchi;
(K)Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa.

Somo la 2

Mdo 13:22-26

Paulo alisema, Mungu alimwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu yote. Katika uzao wake mtu huyo Mungu amewaletea Israeli Mwokozi, yaani, Yesu, kama alivyoahidi; Yohana alipokuwa amekwisha kuwahubiri watu wote wa Israeli habari za ubatizo wa toba, kabla ya kuja kwake. Naye Yohana alipokuwa akimaliza mwendo wake alinena, Mwanidhani mimi kuwa nani? Mimi siye. Lakini, angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye mimi sistahili kumlegezea viatu vya miguu yake. Ndugu zangu, wana wa ukoo wa Ibrahimu, na hao miongoni mwenu wanaomcha Mungu, kwetu sisi neno la wokovu huu limepelekwa.

Shangilio

Lk 1:76

Aleluya, aleluya
Nawe, mtoto, utaitwa nabii wake Aliye juu, Kwa maana utatangulia mbele za uso wa Bwana umtengenezee njia zake;
Aleluya

Injili

Lk 1:57-66, 80

Ikawa, siku za kuzaa kwake Elisabeti zilipotimia, alizaa mtoto mwanamume. Wakasikia jirani zake na jamaa zake ya kwamba Bwana amemwongezea rehema zake, wakafurahi pamoja naye. Ikawa siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto; wakataka kumpa jina la babaye, Zakaria. Mamaye akajibu akasema La, sivyo; bali, ataitwa Yohana. Wakamwambia, Hapana mtu katika jamaa zako aitwaye jina hilo. Wakamwashiria babaye wajue atakavyo kumwita. Akataka kibao, akaandika ya kwamba, Jina lake ni Yohana. Wakastaajabu wote. Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kunena akimsifu Mungu. Wakaingiwa na hofu wote waliokuwa wakikaa karibu nao; na mambo hayo yote yakatangazwa katika nchi yote ya milima milima ya Uyahudi. Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli.

Maoni


Ingia utoe maoni