Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya 6 ya Mwaka (Jumatatu, Februari 17, 2020)  

Somo la 1

Yak 1:1-11

Yakobo, mtumwa wa Mungu, na Bwana Yesu Kristo, kwa kabila kumi na mbili waliotawanyika; salamu. Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno. Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa. Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yoyote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lillilochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana. Mtu wa nia mbili husitasita katika njia zake zote. Lakini ndugu asiye na cheo na afurahi kwa kuwa ametukuzwa; bali tajiri kwa kuwa ameshushwa; kwa maana kama ua la majani atatoweka. Maana jua huchomoza kwa hari, huyakausha majani; ua lake huanguka, uzuri wa umbo lake hupotea; vivyo hivyo naye tajiri atanyauka katika njia zake.

Wimbo wa Katikati

Zab 119:67, 68, 71, 72, 75, 76

Kabla sijateswa mimi nalipotea,
Lakini sasa nimelitii neno lako.
Wewe U mwema na mtenda mema,
Unifundishe amri zako.
(K) Rehema zako, ee Bwana, zinijie nipate kuishi.

Ilikuwa vema kwangu kuwa naliteswa,
Nipate kujifunza amri zako.
Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu,
Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.
(K) Rehema zako, ee Bwana, zinijie nipate kuishi.

Najua ya kuwa hukumu zako ni za haki,
Ee Bwana, na kwa uaminifu umenitesa.
Nakuomba, fadhili zako ziwe faraja kwangu,
Sawasawa na ahadi yako kwa mtumishi wako.
(K) Rehema zako, ee Bwana, zinijie nipate kuishi.

Shangilio

Yn 14:6

Aleluya, aleluya,
Bwana asema: Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya.

Injili

Mk 8:11-13

Walitokea Mafarisayo, wakaanza kuhojiana na Yesu; wakitafuta kwake ishara itokayo mbinguni; wakimjaribu. Akaugua rohoni mwake, akasema, Mbona kizazi hiki chatafuta ishara? Amin, nawaambieni, Hakitapewa ishara kizazi hiki. Akawaacha akapanda tena chomboni, akaenda zake hata ng’ambo.

Maoni


Ingia utoe maoni