Masomo ya Misa
Jumatatu baada ya Epifania (Jumatatu, Januari 06, 2020)
1Yoh 3:22-4:6
Wapenzi: Lolote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake. Na hii ndiyo amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo, na kupendana sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri. Naye azishikaye amri zake hukaa ndani yake yeye, naye ndani yake, kwa huyo Roho aliyetupa. Wapenzi, masiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani. Katika hili mwamjua Roho wa Mungu; kila roho ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu. Na kil aroho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani. Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu; nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia. Hao ni wa dunia; kwa hiyo wanena ya dunia na dunia huwasikia. Sisi twatokana na Mungu. Yeye amjuaye Mungu atusikia; yeye asiyetokana na Mungu hatusikii. Katika hili twamjua Roho wa kweli, na roho ya upotevu.
Zab 2:7-8, 10-11
Nitaihubiri amri; Bwana aliniambia,
Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa.
Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako,
Na miisho ya dunia kuwa milki yako.
(K) Nitakupa mataifa kuwa urithi wako.
Na sasa, enyi wafalme, fanyeni akili,
Enyi waamuzi wa dunia, mwadibiwe.
Mtumikieni Bwana kwa kicho;
Shangilieni kw akutetemeka.
(K) Nitakupa mataifa kuwa urithi wako.
Mt 4:16
Aleluya, aleluya.
Watu wale waliokaa katika giza wameona mwanga mkuu, Nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti mwanga umewazukia.
Aleluya.
Mt 4:12-17, 23-25
Siku ile, Yesu aliposikia ya kwamba Yohane amefungwa, alikwenda zake mpaka Galilaya; akatoka Nazareti, akaja akakaa Kapernaumu, mji ulioko pwani, mipakani mwa Zabuloni na Naftali: ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Nchi ya Zabuloni nan chi ya Naftali, Njia ya bahari, ng’ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa, Watu wale waliokaa katika giza. Wameona mwanga mkuu, nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti mwanga umewazukia. Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. Naye alikuwa akizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu. Na habari zake zikaenea katika Shamu yote; wakamletea wote waliokuwa hawawezi, walioshikw ana maradhi mbalimbali na mteso, wenye pepo, na wenye kifafa, na wenye kupooza; akawaponya. Na makutano mengi wakamfuata, kutoka Galilaya, na Dekapoli, na Yerusalemu, na Uyahudi, na ng’ambo ya Yordani.
Maoni
Ingia utoe maoni