Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne Oktava ya Kuzaliwa Bwana (Jumanne, Desemba 31, 2019)  

Somo la 1

1Yoh 2:18-21

Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho. Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wa kwetu, wangalikaa pamoja nasi. Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote wa kwetu. Nanyi mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote. Sikuwaandikia ninyi kwa sababu hamwijui iliyo kweli, bali kwa sababu mwaijua, tena kwamba hapana uongo wowote utokao katika hiyo kweli.

Wimbo wa Katikati

Zab 96:1-2, 11-13

Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Mwimbieni Bwana, nchi yote.
Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake,
Tangazeni wokovu wake siku kwa siku.
(K) Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie.

Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie,
Bahari na ivume na vyote viijazavyo,
Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo,
Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha;
Mbele za Bwana, kwa maana anakuja,
Kwa maana anakuja aihukumu nchi.
(K) Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie.

Atauhukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa uaminifu wake.
(K) Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie.

Shangilio

Ebr 1:1-2

Aleluya, aleluya
Baada ya Mungu kusema zamani mara nyingi na kwa namna ningi na baba zetu kwa kinywa cha manabii, siku hizi zilizo za mwisho amesema nasi kwa kinywa cha Mwana.
Aleluya.

Injili

Yn 1:1-18

Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza. Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru. Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli. Yohane alimshuhudia, akapaza sauti yake akasema, Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Ajaye nyuma yangu amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema. Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua.

Maoni


Ingia utoe maoni