Masomo ya Misa
Jumatatu ya 3 ya Majilio (Jumatatu, Desemba 16, 2019)
Hes 24:2-7, 15-17
Siku zile Balaamu akainua macho yake akawaona Israeli wamekaa kabila kabila; roho ya Mungu ikamjia. Akatunga mithali yake, akasema, Balaamu mwana wa Beori asema, Yule mtu aliyefumbwa macho asema; Asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu, Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho; Mahema yako ni mazuri namna gani, Ee Yakobo, Maskani zako, Ee Israeli! Mfano wa bonde zimetandwa, Mfano wa bustani kando ya mto, Mfano wa mishubiri aliyoipanda Bwana, Mfano wa mierezi kando ya maji. Maji yatafurika katika ndoo zake, Na mbegu zake zitakuwa katika maji mengi. Na mfalme wake ataadhimishwa kuliko Agagi, Na ufalme wake utatukuzwa. Akatunga mithali yake akasema, Balaamu mwana wa Beori asema, Yule mtu aliyefumbwa macho asema, Asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu, Na kuyajua maarifa yake Aliye Juu. Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho, Namwona, lakini si sasa; Namtazama, lakini si karibu; Nyota itatokea katika Yakobo Na fimbo ya enzi itainuka katika Israeli;
Zab 25:4-6, 7b-9
Ee Bwana, unijulishe njia zako,
Unifundishe mapito yako,
Uniongoze katika kweli yako, Na kunifundisha.
Maana Wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu,
Nakungoja Wewe mchana kutwa.
(K)Ee Bwana unijulishe njia zako.
Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako,
Maana zimekuwako tokea zamani.
Unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako,
Ee Bwana kwa ajili ya wema wako.
(K)Ee Bwana unijulishe njia zako.
Bwana yu mwema, mwenye adili,
Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
Wenye upole atawaongoza katika hukumu,
Wenye upole atawafundisha njia yake.
(K)Ee Bwana unijulishe njia zako.
Zab 85:7
Aleluya, aleluya,
Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako, utupe wokovu wako.
Aleluya.
Mt 21:23-27
Siku ile Yesu alipokwisha kuingia hekaluni, wakuu wa makuhani na wazee wa watu wakamwendea alipokuwa akifundisha, wakasema, Ni kwa amri gani unatenda mambo haya? Naye ni nani aliyekupa amri hii? Yesu akajibu akawaambia, Na mimi nitawauliza neno moja; ambalo mkinijibu, nami nitawaambia ni kwa amri gani ninatenda haya. Ubatizo wa Yohana ulitoka wapi? Ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu? Wakahojiana wao kwa wao, wakisema, Tukisema, Ulitoka mbinguni, atatuambia, Mbona basi hamkumwamini? Na tukisema, Ulitoka kwa wanadamu, twaogopa mkutano; maana watu wote wamwona Yohana kuwa ni nabii. Wakamjibu Yesu wakasema, Hatujui. Naye akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa amri gani ninatenda haya.
Maoni
Ingia utoe maoni