Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 2 ya Majilio (Jumapili, Desemba 08, 2019)  

Somo la 1

Isa 11:1-10

Siku ile: litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda. Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana; na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya. Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia. Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza. Ng'ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng'ombe. Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira. Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari. Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu.

Wimbo wa Katikati

Zab 72:1-2, 7-8, 12-13, 17

Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako,
Na mwana wa mfalme haki yako.
Atawaamua watu wako kwa haki,
Na watu wako walioonewa kwa hukumu.
(K) Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.

Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi,
Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.
Na awe na enzi toka bahari hata bahari,
Toka Mto hata miisho ya dunia.
(K) Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.

Kwa maana atamkomboa mhitaji aliapo,
Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi.
Atamhurumia aliye dhaifu na maskini,
Na nafsi za wahitaji ataziokoa.
(K) Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.

Jina lake na lidumu milele,
Pindi ling'aapo jua jina lake liwe na wazao;
Mataifa yote na wajibariki katika yeye, Na kumwita heri.
(K) Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.

Somo la 2

Rum 15:4-9

Ndugu zangu, yote yaliyotangulia kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha sisi; ili kwa saburi na faraja ya maandiko tupate kuwa na tumaini. Na Mungu mwenye saburi na faraja awajalie kunia mamoja ninyi kwa ninyi, kwa mfano wa Kristo Yesu; ili kwa moyo mmoja na kwa kinywa kimoja mpate kumtukuza Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa hiyo mkaribishane ninyi kwa ninyi, kama naye Kristo alivyotukaribisha, ili Mungu atukuzwe. Kwa maana nasema, ya kwamba Kristo amefanyika mhudumu wa agano la kutahiriwa kwa ajili ya kweli ya Mungu, kusudi azithibitishe ahadi walizopewa baba zetu; tena ili Mataifa wamtukuze Mungu kwa ajili ya rehema zake; kama ilivyoandikwa, Kwa hiyo nitakushukuru kati ya Mataifa, Nami nitaliimbia jina lako.

Shangilio

Lk 3:4,6

Aleluya, aleluya
Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake,na wote wenye mwili watauona wokovu wa Mungu.
Aleluya

Injili

Mt 3:1-12

Siku zile aliondokea Yohana Mbatizaji akihubiri katika nyika ya Uyahudi, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. Kwa sababu huyo ndiye aliyenenwa na nabii Isaya, akisema, Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake. Naye Yohana mwenyewe alikuwa na vazi lake la singa za ngamia, na mshipi wa ngozi kiunoni mwake; na chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu. Ndipo walipomwendea Yerusalemu, na Uyahudi wote, na nchi zote za kandokando ya Yordani; naye akawabatiza katika mto wa Yordani, huku wakiziungama dhambi zao. Hata alipoona wengi miongoni mwa Mafarisayo na Masadukayo wakiujia ubatizo wake, aliwaambia, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? Basi zaeni matunda yapasayo toba; wala msiwaze mioyoni mwenu kwamba, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba Mungu aweza katika mawe haya kumwinulia Ibrahimu watoto. Na shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni. Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. Ambaye pepeto lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake; na kuikusanya ngano yake ghalani, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.

Maoni


Ingia utoe maoni