Masomo ya Misa
Alhamisi ya 30 ya Mwaka (Alhamisi, Oktoba 31, 2019)
Rum 8:31-39
Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.
Zab 109:21-22, 26-27, 30-31
Na Wewe, MUNGU, Bwana, unitendee kwa ajili ya jina lako,
Kwa kuwa fadhili zako ni njema uniokoe.
Kwa maana mimi ni mnyonge na mhitaji,
Na moyo wangu umejeruhi ndani yangu.
(K) Ee Bwana, uniokoe sawasawa na fadhili zako.
Ee Bwana, Mungu wangu, unisaidie,
Uniokoe sawasawa na fadhili zako.
Nao wakajue ya kuwa ndio mkono wako;
Wewe, Bwana, umeyafanya hayo.
(K) Ee Bwana, uniokoe sawasawa na fadhili zako.
Nitamshukuru Bwana kwa kinywa changu,
Naam, nitamsifu katikati ya mkutano.
Maana atasimama mkono wa kuume wa mhitaji
Amwokoe na wanaoihukumu nafsi yake.
(K) Ee Bwana, uniokoe sawasawa na fadhili zako.
Lk 13:31-35
Siku moja, Mafarisayo kadha wa kadha walimwendea, wakamwambia, Toka hapa, uende mahali pengine, kwa sababu Herode anataka kukuua. Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika. Pamoja na hayo imenipasa kushika njia yangu leo na kesho na kesho kutwa; kwa kuwa haimkini nabii aangamie nje ya Yerusalemu. Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga kwa mawe waliotumwa kwako, mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako kama vile kuku avikusanyavyo vifaranga vyake chini ya mbawa zake, wala hamkutaka. Angalieni, mmeachiwa nyumba yenu! Nami nawaambia, Hamtaniona tena kamwe, hata mtakaposema, Amebarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.
Maoni
Ingia utoe maoni