Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 30 ya Mwaka (Jumapili, Oktoba 27, 2019)  

Somo la 1

Ybs 35:12-14,16-19

Kwa kuwa Bwana ndiye mhukumu wala hakijali cheo cha mtu. Hatamkubali ye yote juu ya maskini, naye ataisikiliza sala yake aliyedhulumiwa. Hatayadharau kamwe malalamiko ya yatima, wala ya mjane amwelezapo habari zake. Malalamiko yakealiyeonewa yatapata kukubaliwa, na dua yake itafika hima mbinguni. Sala yake mnyenyekevu hupenya mawingu; wala haitatulia hata itakapowasili; wala haitaondoka hata Aliye juu atakapoiangalia, akaamua kwa adili, akatekeleza hukumu. Wala Bwana hatalegea, walahatakuwa mvumilivu kwa wanadamu.

Wimbo wa Katikati

Zab 34:1-2, 16-18, 22

Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.
(K) Maskini huyu aliita Bwana akasikia

Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya,
Aliondoe kumbukumbu lao duniani.
Walilia, naye Bwana akasikia,
Akawaponya na taabu zao zote.
(K) Maskini huyu aliita Bwana akasikia

Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo,
Na waliopondeka roho huwaokoa.
Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake,
Wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao.
(K) Maskini huyu aliita Bwana akasikia

Somo la 2

2 Tim 4:6-8, 16-18

Mimi sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika. Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake. Katika jawabu langu la kwanza hakuna mtu aliyesimama upande wangu, bali wote waliniacha; naomba wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo. Lakini Bwana alisimama pamoja nami akanitia nguvu, ili kwa kazi yangu ule ujumbe utangazwe kwa utimilifu, hata wasikie Mataifa yote; nami nikaokolewa katika kinywa cha simba. Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye milele na milele. Amina.

Shangilio

Yn 8:12

Aleluya, aleluya
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana, Yeye anifuataye atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya

Injili

Lk 18:9-14

Yesu aliwaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.

Maoni


Ingia utoe maoni