Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya 29 ya Mwaka (Jumatatu, Oktoba 21, 2019)  

Somo la 1

Rum 4:20-25

Ibrahimu akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutokuamini, bali alitiwa nguvu kwa imani, akimtukuza Mungu; huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi. Kwa hiyo ilihesabiwa kwake kuwa ni haki. Walakini haikuandikwa kwa ajili yake tu kwamba ilihesabiwa kwake; bali na kwa ajili yetu sisi mtakaohesabiwa vivyo hivyo, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu katika wafu; ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki.

Wimbo wa Katikati

Lk 1:69-75

Ametusimamishia pembe ya wokovu Katika mlango wa Daudi, mtumishi wake.
Kama alivyosema tangu mwanzo Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu;
(K) Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli

Tuokolewe na adui zetu Na mikononi mwao wote wanaotuchukia;
Ili kuwatendea rehema baba zetu,
Na kulikumbuka agano lake takatifu;
(K) Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli

Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu,
Ya kwamba atatujalia sisi,
Tuokoke mikononi mwa adui zetu,
Na kumwabudu pasipo hofu,
Kwa utakatifu na kwa haki Mbele zake siku zetu zote.
(K) Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli

Injili

Lk 12:13-21

Mtu mmoja katika mkutano alimwambia Yesu, Mwalimu, mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu. Akamwambia, Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu? Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo. Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.

Maoni


Ingia utoe maoni