Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 28 ya Mwaka (Alhamisi, Oktoba 17, 2019)  

Somo la 1

Rum 3:21-30

Haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; ina shuhudiwa na torati na manabii; ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya Imani katika yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti; kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya Imani katika damu yake, ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa; apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yeye amwaminiye Yesu. Ku wapi, basi, kujisifu? Kumefungiwa nje. Kwa sheria ya namna gani? Kwa sheria ya matendo? La! Bali kwa sheria ya Imani. Basi, twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa Imani pasipo matendo ya sheria. Au je! Mungu ni Mungu wa Wayahudi tu? Siye Mungu wa Mataifa pia? Naam, ni Mungu wa Mataifa pia; kama kwa kweli Mungu ni mmoja.

Wimbo wa Katikati

Zab 130:1-6

Ee Bwana, toka vilindini nimekulilia,
Bwana, uisikie sauti yangu.
Masikio yako na yaisikilize,
Sauti ya dua zangu.
(K) Kwa Bwana kuna fadhili na ukombozi mwingi.

Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu,
Ee Bwana, nani angesimama?
Lakini kwako kuna msamaha,
Ili Wewe uogopwe.
(K) Kwa Bwana kuna fadhili na ukombozi mwingi.

Nimemngoja Bwana, roho yangu imemngoja;
Na neno lake nimelitumainia.
Nafsi yangu inamngoja Bwana,
Kuliko walinzi waingojavyo asubuhi,
Naam, walinzi waingojao asubuhi.
(K) Kwa Bwana kuna fadhili na ukombozi mwingi.

Shangilio

Zab 119:28,33

Aleluya, aleluya,
Unitie nguvu sawasawa na neno lako, Ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako.
Aleluya.

Injili

Lk 11:47-54

Yesu aliwaambia wanasheria: Ole wenu, kwa kuwa mwajenga maziara ya manabii, na baba zenu ndio waliowaua. Basi, mwashuhudia na kuziridhia kazi za baba zenu; kwa kuwa wao waliwaua nanyi mwawajengea maziara. Na kwa sababu hiyo hekima ya Mungu ilisema, Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao watawaua baadhi yao na kuwafukuza, ili kwa kizazi hiki itakwe damu ya manabii wote, iliyomwagika tangu kupigwa msingi wa ulimwengu; tangu damu ya Habili hata damu ya Zakaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na hekalu. Naam, nawaambieni ya kwamba itatakwa kwa kizazi hiki. Ole wenu, enyi wanasheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia. Alipotoka humo, waandishi na Mafarisayo walianza kumsonga vibaya, na kumchokoza kwa maswali mengi, wakimvizia, ili wapate neno litokalo kinywani mwake.

Maoni


Ingia utoe maoni