Masomo ya Misa
Jumanne ya 23 ya Mwaka (Jumanne, Septemba 10, 2019)
Kol 2:6-15
Kama mlivyompokea Kristo Yesu Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye; wenye shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa Imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani. Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo. Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili. Na ninyi mmetimilika katika yeye aliye kichwa cha enzi yote na mamlaka. Katika yeye mmetahiriwa kwa tohara isiyofanyika kwa mikono, kwa kuuvua mwili wa nyama, kwa tohara ya Kristo. Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu. Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutotahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote. Akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa kwa kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.
Zab 145:1-2, 8-11
Ee Mungu wangu Mfalme, nitakutukuza,
Nitalihimidi jina lako milele na milele,
Kila siku nitakuhimidi,
Nitalisifu jina lako milele na milele.
(K) Bwana ni mwema kwa watu wote.
Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma,
Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema
Bwana ni mwema kwa watu wote,
Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote.
(K) Bwana ni mwema kwa watu wote.
Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
Wataunena utukufu wa ufalme wako,
Na kuuhadithia uweza wako.
(K) Bwana ni mwema kwa watu wote.
Zab 111:7, 8
Aleluya, aleluya,
Maagizo yako yote, Ee Bwana, ni amini, yamethibitika milele na milele.
Aleluya.
Lk 6:12–19
Yesu aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu. Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume; Simoni, aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohane, na Filipo na Bartolomayo, na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote, na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti. Akashuka pamoja nao, akasimama mahali tambarare, pamoja na wanafunzi wake wengi, na makutano makubwa ya watu waliotoka Uyahudi wote na Yerusalemu, na pwani ya Tiro na Sidoni; waliokuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao; na wale waliosumbuliwa na pepo wachafu; waliponywa. Na makutano yote walikuwa wakitaka kumgusa, kwa sababu uweza ulikuwa ukimtoka ukiwaponya wote.
Maoni
Ingia utoe maoni