Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya 22 ya Mwaka (Jumatatu, Septemba 02, 2019)  

Somo la 1

1The 4:13-17

Ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini. Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti. Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele.

Wimbo wa Katikati

Zab 96:1, 3-5, 11-13

Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Mwimbieni Bwana, nchi yote.
Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
Na watu wote habari za maajabu yake.
(K) Bwana anakuja aihukumu nchi.

Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kusifiwa sana.
Na wa kuhofiwa kuliko miungu yote.
Maana miungu yote ya watu si kitu,
Lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu.
(K) Bwana anakuja aihukumu nchi.

Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie,
Bahari na ivume na vyote viijazavyo,
Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo,
Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha;
(K) Bwana anakuja aihukumu nchi.

Mbele za Bwana, kwa maana anakuja,
Kwa maana anakuja aihukumu nchi.
Atauhukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa uaminifu wake.
(K) Bwana anakuja aihukumu nchi.

Injili

Lk 4:16-30

Yesu alienda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu. Wakamshuhudia wote, wakiyastaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake, wakasema, Huyu siye mwana wa Yusufu? Akawaambia, Hapana shaka mtaniambia mithali hii, Tabibu, jiponye nafsi yako; mambo yote tuliyosikia kwamba yametendeka Kapernaumu, yatende na hapa pia katika nchi yako mwenyewe. Akasema, Amin, nawaambia ya kwamba, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe. Lakini, kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima; wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. Tena, palikuwa na wenye ukoma wengi katika Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana aliyetakaswa ila Naamani, mtu wa Shamu. Wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika sinagogi walipoyasikia hayo. Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini; lakini yeye alipita katikati yao, akaenda zake.

Maoni


Ingia utoe maoni