Masomo ya Misa
Dominika ya 21 ya Mwaka (Jumapili, Agosti 25, 2019)
Isa 66:18-21
Bwana asema hivi, Nami nayajua matendo yao na mawazo yao; wakati unakuja nitakapokusanya mataifa yote na lugha zote; nao watakuja, nao watauona utukufu wangu. Nami nitaweka ishara kati yao, nami nitawatuma hao waliookoka kwa mataifa, Tarshishi, na Puli, na Ludi, wavutao upinde, kwa Tubali na Yavani, visiwa vilivyo mbali; watu wasioisikia habari yangu, wala kuuona utukufu wangu; nao watahubiri utukufu wangu katika mataifa. Nao watawaleta ndugu zenu wote kutoka mataifa yote, kuwa sadaka kwa Bwana, juu ya farasi, na katika magari, na katika machela, na juu ya nyumbu, na juu ya wanyama wepesi, mpaka mlima wangu mtakatifu Yerusalemu, asema Bwana; kama vile wana wa Israeli waletavyo sadaka yao nyumbani kwa Bwana katika chombo safi. Na baadhi ya hao nitawatwaa kuwa makuhani na Walawi, asema Bwana.
Zab 117
Aleluya.
Enyi mataifa yote, msifuni Bwana,
Enyi watu wote, mhimidini.
(K) Enendeni ulimwenguni mwote, Mkaihubiri Injili.
Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu,
Na uaminifu wa Bwana ni wa milele.
(K) Enendeni ulimwenguni mwote, Mkaihubiri Injili.
Ebr 12:5-7, 11-13
Tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, Wala usizimie moyo ukikemewa naye; Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye. Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye? Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani. Kwa hiyo inyosheni mikono iliyolegea na magoti yaliyopooza, mkaifanyie miguu yenu njia za kunyoka, ili kitu kilicho kiwete kisipotoshwe, bali afadhali kiponywe.
Yn 17:17
Aleluya, aleluya,
Maneno yako ndiyo kweli Ee Bwana, Utatukase sisi kwa ile kweli.
Aleluya
Lk 13:22-30
Yesu alikuwa akipita katika miji na vijiji, akifundisha, katika safari yake kwenda Yerusalemu. Mtu mmoja akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akawaambia, Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze. Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako; ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu. Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu. Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje. Nao watakuja watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu. Na tazama, wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.
Maoni
Ingia utoe maoni