Masomo ya Misa
Jumanne ya 19 ya Mwaka (Jumanne, Agosti 13, 2019)
Kum 31:1-8
Musa alienda akawaambia Waisraeli maneno haya yote. Akawaambia, Mimi leo ni mwenye miaka mia na ishirini; siwezi tena kutoka na kuingia, na Bwana ameniambia, Hutavuka mto huu Yordani. Bwana Mungu wako, ndiye atakayevuka mbele yako, atawaangamiza mataifa haya mbele yako, nawe utawamiliki; na Yoshua atavuka mbele yako, kama Bwana alivyonena. Na Bwana atawatenda hao kama vile alivyowatenda Sihoni na Ogu, wafalme wa Waamori, na nchi yao, ambao aliwaharibu. Naye Bwana atawatia mikononi mwenu, nanyi mtawatenda kadiri ya amri ile niliyowaamuru. Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu; kwa maana Bwana, Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha. Musa akamwita Yoshua, akamwambia machoni pa Israeli wote, Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana utakwenda pamoja na watu hawa hata nchi Bwana aliyowaapia baba zao, ya kwamba atawapa; nawe utawarithisha. Naye Bwana, yeye ndiye atakayekutangulia, atakuwa pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha; usiogope wala usifadhaike.
Kum 32:3-4, 7-9, 12
Maana nitalitangaza Jina la Bwana;
Mpeni ukuu Mungu wetu.
Yeye Mwamba, kazi yake ni kamilifu;
Maana, njia zake zote ni haki.
(K) Sehemu ya Bwana ni watu wake
Kumbuka siku za kale,
Tafakari miaka ya vizazi vingi;
Mwulize baba yako, naye atakuonyesha;
Wazee wako, nao watakuambia.
(K) Sehemu ya Bwana ni watu wake
Yeye Aliye Juu alipowapa mataifa urithi wao,
Alipowabagua wanadamu,
Aliweka mipaka ya watu Kwa kadiri ya hesabu ya wana wa Israeli.
(K) Sehemu ya Bwana ni watu wake
Maana, sehemu ya Bwana ni watu wake,
Yakobo ni kura ya urithi wake.
Bwana peke yake alimwongoza,
Wala hapakuwa na mungu mgeni pamoja naye.
(K) Sehemu ya Bwana ni watu wake
Mt 18: 1-5, 10, 12-14
Wanafunzi walimwendea Yesu wakisema, Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni. Na ye yote atakayempokea mtoto mmoja mfano wa huyu kwa jina langu, anipokea mimi; Angalieni msidharau mmojawapo wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba malaika wao mbinguni siku zote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni. Mwaonaje? Mtu akiwa na kondoo mia, mmoja akampotea, je! Hawaachi wale tisa na tisini, akaenda milimani, na kumtafuta yule aliyepotea? Vivyo hivyo haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee.
Maoni
Ingia utoe maoni