Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Kumbukumbu ya Mtakatifu Martha (Jumatatu, Julai 29, 2019)  

Somo la 1

Kut 32:15-24, 30-34

Musa aligeuka akashuka katika mlima, na zile mbao mbili za mawe mikononi mwake; mbao zilizoandikwa pande zote mbili, upande huu na upande huu ziliandikwa. Na zile mbao zilikuwa kazi ya Mungu nayo maandiko yalikuwa maandiko ya Mungu, yaliyochorwa katika zile mbao. Na Yoshua aliposikia kelele za watu walipokuwa wakipiga kelele, akamwambia Musa, Kuna kelele ya vita maragoni. Akasema, Hiyo si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushinda vitani, wala si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushindwa; bali kelele za watu waimbao ndizo ninazozisikia mimi. Hata alipoyakaribia marago akaiona ile ndama, na ile michezo. Hasira ya Musa ikawaka, akazitupa zile mbao mikononi mwake, akazivunja chini ya mlima. Akaitwaa ile ndama waliyoifanya, akaichoma moto, akaisaga hata ikawa mavumbi, akainyunyiza juu ya maji, akawanywesha wana wa Israeli. Musa akamwambia Haruni Watu hawa wamekufanyani hata ukaleta dhambi hii kuu juu yao? Haruni akasema, Hasira ya bwana wangu isiwake, wewe unawajua watu hawa, ya kuwa wamejielekeza kwa mabaya. Maana waliniambia, Katufanyie miungu, itakayokwenda mbele yetu, kwa maana mtu huyo Musa, aliyetutoa katika nchi ya Misri, hatujui yaliyompata. Nikawaambia, Mtu ye yote aliye na dhahabu na aivunje; basi wakanipa, nami nikaitupa ndani ya moto, akatoka ndama huyu. Hata asubuhi yake Musa akawaambia watu, Mmetenda dhambi kuu; na sasa nitakwenda juu kwa Bwana, labda nitafanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu. Musa akarejea kwa Bwana akasema, Aa! Watu hawa wametenda dhambi kuu wamejifanyia miungu ya dhahabu. Walakini sasa, ikiwa utawasamehe dhambi yao -- na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichoandika. Bwana akamwambia Musa, Mtu ye yote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu. Basi sasa uende ukawaongoze watu hawa mpaka mahali pale ambapo nimekwambia habari zake; tazama, malaika wangu atakutangulia; pamoja na hayo siku nitakayowajilia nitawapatiliza kwa ajili ya dhambi yao.

Wimbo wa Katikati

Zab 106:19-23

Walifanya ndama huko Horebu,
Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka.
Wakaubadili utukufu wao Kuwa mfano wa ng'ombe mla majani.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema.

Wakamsahau Mungu, mwokozi wao,
Aliyetenda makuu katika Misri.
Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu,
Mambo ya kutisha penye bahari ya Shamu.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema.

Akasema ya kuwa atawaangamiza Kama Musa,
mteule wake, asingalisimama,
Mbele zake kama mahali palipobomoka,
Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema.

Injili

Mt 13:31-35

Yesu aliwatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake; nayo ni ndogo kuliko mbegu zote; lakini ikiisha kumea, huwa kubwa kuliko mboga zote, ikawa mti, hata nyuni wa angani huja na kukaa katika matawi yake. Akawaambia mfano mwingine; Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyoitwaa mwanamke, akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachachwa wote pia. Hayo yote Yesu aliwaambia makutano kwa mifano; wala pasipo mfano hakuwaambia neno; ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Nitafumbua kinywa changu kwa mifano, Nitayatamka yaliyositirika tangu awali.

Maoni


Ingia utoe maoni