Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 16 ya Mwaka (Jumapili, Julai 21, 2019)  

Somo la 1

Mwa 18:1-10

Bwana alimtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari. Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi, akasema, Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako. Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu. Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, iwapo mmemjia mtumwa wenu. Wakasema, Haya, fanya kama ulivyosema. Basi Ibrahimu akaenda hima hemani kwa Sara, akasema, Himiza vipimo vitatu vya unga safi, uukande, ufanye mikate. Ibrahimu akapiga mbio kwenda kundini, akaleta ndama wa ng’ombe aliye laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akahimiza kuiandaa. Akatwaa siagi na maziwa, na ndama aliyoiandaa, akawaandikia mbele yao, akasimama karibu nao chini ya mti, nao wakala. Wakamwambia, Yu wapi Sara mkeo? Akasema, Yumo hemani. Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati uu huu mwakani. na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume.

Wimbo wa Katikati

Zab 15

Bwana, ni nani atakayefanya maskani yake
Katika kilima chako kitakatifu?
Ni yeye aendaye kwa ukamilifu,
Na kutenda haki;
Asemaye kweli kwa moyo wake,
Asiyesingizia kwa ulimi wake.
(K) Bwana, ni nani atakayekaa katika hema yako

Yeye ambaye hakumtenda mwenziwe mabaya,
Wala hakumsengenya jirani yake.
Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa,
Bali huwaheshimu wamchao Bwana.
(K) Bwana, ni nani atakayekaa katika hema yako

Yeye ambaye hakutoa fedha yake apate kula riba,
Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia.
Mtu atendaye mambo hayo
Hataondoshwa milele.
(K) Bwana, ni nani atakayekaa katika hema yako

Somo la 2

Kol 1:24-28

Nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu; tena nayatimiliza katika mwili wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani, kanisa lake, ambalo nimefanywa mhudumu wake, sawasawa na uwakili wa Mungu, niliopewa kwa faida yenu, nilitimize neno la Mungu; siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake; ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa, nao ni Kristo ndani yenu; tumaini la utukufu; ambaye sisi tunamhubiri habari zake, tukimwonya kila mtu, na kumfundisha kila mtu katika hekima yote, tupate kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo.

Shangilio

Yn 14:23

Aleluya, aleluya,
Mtu akinipenda, atalishika neno langu; Na Baba yangu atampenda; Nasi tutakuja kwake.
Aleluya.

Injili

Lk 10:38-42

Ikawa katika kuenenda kwao Yesu aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake. Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake. Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie. Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.

Maoni

Ernest Gerdath

Hakika nimejifunza kitu kupitia masomo ya leo

Ernest Gerdath

Hakika nimejifunza kitu kupitia masomo ya leo

Ingia utoe maoni