Masomo ya Misa
Jumatano ya 15 ya Mwaka (Jumatano, Julai 17, 2019)
Kut 3:1-6, 9-12
Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu. Malaika wa Bwana akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea. Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei. Bwana alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa. Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapa unaposimama ni nchi takatifu. Tena akasema, Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu. Bwana akasema: Tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa. Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, nikawatoe wana wa Israeli watoke Misri? Akasema, Bila shaka mimi nitakuwa pamoja nawe; na dalili ya kuwa nimekutuma ndiyo hii; utakapokuwa umekwisha kuwatoa hao watu katika Misri, mtamwabudu Mungu katika mlima huu.
Zab 103:1-4, 6-7
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Naam vyote vilivyo ndani yangu
Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote.
(K) Bwana amejaa huruma na neema.
Akusamehe maovu yako yote,
Akuponya magonjwa yako yote.
Aukomboa uhai wako na kaburi,
Akutia taji ya fadhili na rehema.
(K) Bwana amejaa huruma na neema.
Bwana ndiye afanyaye mambo ya haki,
Na hukumu kwa wote wanaoonewa.
Akimjulisha Musa njia zake,
Wana wa Israeli matendo yake.
(K) Bwana amejaa huruma na neema.
Zab 19:8
Aleluya, aleluya,
Amri ya Bwana ni safi, huyatia macho nuru.
Aleluya.
Mt 11:25–27
Wakati ule Yesu alijibu akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na baba yangu; wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na yenyote ambaye Mwana apenda kumfunulia.
Maoni
Ingia utoe maoni