Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 10 ya Mwaka (Ijumaa, Juni 14, 2019)  

Somo la 1

2Kor 4:7–15

Tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu. Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi; sikuzote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu. Kwa maana sisi tulio hai, sikuzote twatolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu ipatikanayo na mauti. Basi hapo mauti hufanya kazi ndani yetu, bali uzima ndani yenu. Lakini kwa kuwa tuna roho ile ile ya Imani; kama ilivyoandikwa, Naliamini, na kwa sababu hiyo nalinena; sisi nasi twaamini, na kwa sababu hiyo twanena; tukijua ya kwamba yeye aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi nasi pamoja na Yesu, na kutuhudhurisha pamoja nanyi. Kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe.

Wimbo wa Katikati

Zab 116:10–11, 15–19

Naliamini, kwa maana nitasema,
Mimi naliteswa sana.
Mimi nalisema kwa haraka yangu,
Wanadamu wote ni waongo.
(K) Nitakutolea dhabihu ya kushukuru, Ee Bwana.

Ina thamani machoni pa Bwana
Mauti ya wacha Mungu wake.
Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako,
Mtumishi wako, mwana na mjakazi wako,
Umevifungua vifungo vyangu.
(K) Nitakutolea dhabihu ya kushukuru, Ee Bwana.

Nitakutolea dhabihu ya kushukuru;
Na kulitangaza jina la Bwana;
Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
Naam, mbele ya watu wake wote.
(K) Nitakutolea dhabihu ya kushukuru, Ee Bwana.

Shangilio

2Tim 1:10

Aleluya, aleluya.
Mwokozi wetu Yesu Kristu alibatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika kwa Injili.
Aleluya.

Injili

Mt 5:27-32

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake. Jicho alko la kuume likikukosesha, ling’oe ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum. Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee, wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum. Imenenwa pia, Mtu akimwacha mkewe, na ampe hati ya talaka; lakini mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini.

Maoni


Ingia utoe maoni