Masomo ya Misa
Dominika ya 7 ya Pasaka (Jumapili, Juni 02, 2019)
Mdo 7:55-60a
Stefano akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu. Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu. Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja, wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli. Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu. Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii.
Zab 97:1-2, 6-7, 9
Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie,
Visiwa vingi na vifurahi.
Mawingu na giza vyamzunguka,
Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake.
(K) Bwana ametamalaki, Maana Wewe, Bwana, ndiwe Uliye juu, Juu sana kuliko nchi yote
Mbingu zimetangaza haki yake,
Na watu wote wameuona utukufu wake.
Na waaibishwe wote waabuduo sanamu,
Wajivunao kwa vitu visivyofaa;
Enyi miungu yote, msujuduni Yeye.
(K) Bwana ametamalaki, Maana Wewe, Bwana, ndiwe Uliye juu, Juu sana kuliko nchi yote
Maana Wewe, Bwana, ndiwe Uliye juu,
Juu sana kuliko nchi yote;
Umetukuka sana juu ya miungu yote.
(K) Bwana ametamalaki, Maana Wewe, Bwana, ndiwe Uliye juu, Juu sana kuliko nchi yote
Ufu 22:12-14, 16-17, 20
Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo. Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho. Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake. Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzao wa Daudi, ile nyota yenye kung'aa ya asubuhi. Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure. Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, Naam; naja upesi. Amina; na uje, Bwana Yesu.
Yn 17:20-26
Yesu aliinua macho yake mbinguni akasema: Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi. Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu. Baba mwenye haki, ulimwengu haukukujua; lakini mimi nalikujua, na hao wamejua ya kuwa ndiwe uliyenituma. Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao.
Maoni
Ingia utoe maoni