Masomo ya Misa
Alhamisi ya 5 ya Pasaka (Alhamisi, Mei 23, 2019)
Mdo. 15:7-21
Wakati wa Mtaguso wa Yerusalemu, baada ya hoja nyingi Petro alisimama, akawaambia, Ndugu zangu, ninyi mnajua ya kuwa tangu siku za kwanza Mungu alichagua miongoni mwenu ya kwamba Mataifa walisikie neno la Injili kwa kinywa changu, na kuliamini. Na Mungu, ajuaye mioyo ya watu, akawashuhudia, akiwapa Roho Mtakatifu vile vile kama alivyotupa sisi; wala hakufanya tofauti kati yetu sisi na wao, akiwasafisha mioyo yao kwa imani. Basi sasa mbona mnamjaribu Mungu na kuweka kongwa juu ya shingo za wanafunzi, ambalo baba zetu wala sisi hatukuweza kulichukua. Bali twaamini kwamba tutaokoka kwa neema ya Bwana Yesu vile vile kama wao. Basi mkutano wote wakanyamaza, wakawasikiliza Barnaba na Paulo wakiwapasha habari za ishara na maajabu, ambayo Mungu aliyafanya kwa ujumbe wao katika Mataifa. Na hao walipokwisha kunyamaza Yakobo akajibu, akisema, Ndugu zangu, nisikilizeni. Simeoni ametueleza jinsi Mungu hapo kwanza alivyowaangalia Mataifa ili achague watu katika hao kwa ajili ya jina lake. Na maneno ya manabii yapatana na hayo, kama ilivyoandikwa. Baada ya mambo haya nitarejea, nami nitaijenga tena nyumba ya Daudi iliyoanguka. Nitajenga tena maanguko yake, nami nitaisimamisha; ili wanada- mu waliosalia wamtafute Bwana, na mataifa yote ambao jina langu limetajwa kwao; asema Bwana, ajulishaye hayo tangu milele. Kwa sababu hiyo mimi naamua hivi; Tusiwata- abishe wale waliomgeukia Mungu katika Mataifa; bali tuwaandikie kwamba wajiepushe na unajisi wa sanamu, na uasherati, na nyama zilizosongolewa, na damu. Kwa maana tangu zamani za kale Musa anao watu wahubirio mambo yake; katika kila mji husomwa kila sabato katika masinagogi.
Zab. 96:1-3, 10
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Mwimbieni Bwana nchi yote.
Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake.
(K) Wahubirini mataifa habari za utukufu wake.
Tangazeni wokovu wake siku kwa siku.
Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
Na watu wote habari za maajabu yake.
(K) Wahubirini mataifa habari za utukufu wake.
Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki;
Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike,
Atawahukumu watu kwa adili.
(K) Wahubirini mataifa habari za utukufu wake.
Lk. 24 : 25-26
Aleluya, aleluya,
Ilimpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake.
Aleluya.
Yn. 15:9-11
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu. Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe.
Maoni
Ingia utoe maoni