Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya juma la saba la Mwaka C (Jumatatu, Mei 16, 2016)  

Somo la 1

Yak 3:13-18

N'nani aliye na hekima na ufahamu kwenu? Na aonyeshe kazi zake kwa mwenendo wake mzuri, katika upole wa hekima. Lakini, mkiwa na wivu wenye uchungu na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu, wala msiseme uongo juu ya kweli. Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani. Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya. Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki. Na tunda la haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.

Wimbo wa Katikati

Zab 19:7-9, 14

Sheria ya Bwana ni kamilifu, Huiburudisha nafsi.
Ushuhuda wa Bwana ni amini, Humtia mjinga hekima.
(K)Maagizo ya Bwana, huufurahisha moyo

Maagizo ya Bwana ni ya adili, Huufurahisha moyo.
Amri ya Bwana ni safi, Huyatia macho nuru.
(K)Maagizo ya Bwana, huufurahisha moyo

Kicho cha Bwana ni kitakatifu, Kinadumu milele.
Hukumu za Bwana ni kweli, Zina haki kabisa.
(K)Maagizo ya Bwana, huufurahisha moyo

Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu,
Yapate kibali mbele zako, Ee Bwana, Mwamba wangu, na mwokozi wangu.
(K)Maagizo ya Bwana, huufurahisha moyo

Shangilio

2Tim 1:10


Aleluya, Aleluya
Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili;
Aleluya

Injili

Mk 9:14-29

Yesu na Petro na Yakobo na Yohane walipowafikia wanafunzi, waliona mkutano mkuu wakiwazunguka, na waandishi wakijadiliana nao;mara mkutano wote walipomwona walishangaa, wakamwendea mbio, wakamsalimu. Akawauliza, Mnajadiliana nini nao? Mtu mmoja katika mkutano akamjibu, Mwalimu, nimemleta mwanangu kwako, ana pepo bubu; na kila ampagaapo, humbwaga chini, naye hutoka povu na kusaga meno na kukonda; nikasema na wanafunzi wako wamtoe pepo, wasiweze. Akawajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini? Nichukuliane nanyi hata lini? Mleteni kwangu. Wakamleta kwake; hata alipomwona, mara yule pepo alimtia kifafa; naye akaanguka chini, akagaa-gaa, akitokwa na povu. Akamwuliza babaye, Amepatwa na haya tangu lini? Akasema, Tangu utoto. Na mara nyingi amemtupa katika moto, na katika maji, amwangamize; lakini ukiweza neno lo lote, utuhurumie, na kutusaidia. Yesu akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye. Mara babaye yule kijana akapaza sauti, akasema, Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu. Naye Yesu akiona ya kuwa mkutano unakusanyika mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akamwambia, Ewe pepo bubu na kiziwi, mimi nakuamuru, mtoke huyu, wala usimwingie tena. Akalia, akamtia kifafa sana, akamtoka; naye akawa kama amekufa; hata wengi wakasema, Amekufa. Lakini Yesu akamshika mkono akamwinua naye akasimama. Hata alipoingia nyumbani, wanafunzi wake wakamwuliza kwa faragha, Mbona sisi hatukuweza kumtoa? Akawaambia, Namna hii haiwezi kutoka kwa neno lo lote, isipokuwa kwa kuomba.

Maoni


Ingia utoe maoni