Masomo ya Misa
Ijumaa ya 7 ya Mwaka (Ijumaa, Machi 01, 2019)
Ybs. 6:5 – 17
Maneno matamu yatamzidishia mtu rafiki, na midomo yenye neema itamwongezea wamsalimuo. Wale wenye Amani nawe na wawe na wawe wengi; bali washauri wako mmoja katika elfu. Ukitaka kujipatia rafiki, umpate kwa kumjaribu, wala usiwe na haraka katika kumwamini; yaani, kuna rafiki wakati wa kufaa, ambaye yeye hatadumu wakati wa msiba wako. Tena kuna rafiki ageukaye kuwa adui, anye atakukashifia fitina iletayo lawama. Pia kuna rafiki tena, ambaye anakula memzani pako, bali siku ya mabaya haonekani; wakati wa kufanikiwa kwako atakuwa sawa nawe, na kupiga domo juu ya watumishi wako; lakini ukipatwa na masaibu atakugeua, na kujificha mabli nawe na uso wako. Basi ujitenge na adui zako; tena ujihadhari na rafiki zako. Walakini rafiki aliye amini ndiye ngome; naye aliyempata amepata tunu. Hakuna badala ya rafiki amini, wala uzuri wake hauna bei. Rafiki amini ni kifunga uzima; naye amchaye Mungu atampata. Mcha Mungu hunyosha urafiki wake, kwa maana alivyo yeye mwenyewe ndivyo alivyo na jirani yake.
Zab. 119:12, 16, 18, 27, 34 – 35
Ee Bwana, umehimidiwa,
Unifundishe amri zako.
Nitajifurahisha sana kwa amri zako,
Sitalisahau neno lako.
(K) Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako, Ee Bwana.
Unifumbue macho yangu niyatazame,
Maajabu yatokayo katika sheria yako.
Unifahamishe njia ya mausia yako,
Nami nitayatafakari maajabu yako.
(K) Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako, Ee Bwana.
Unifahamishe nami nitaishika sheria yako,
Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote.
Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako,
Kwa maana nimependezwa nayo.
(K) Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako, Ee Bwana.
Zab. 130:5
Aleluya, aleluya,
Roho yangu inamngoja Bwana, na neno lake nimelitumainia.
Aleluya.
Mk. 10:1-12
Yesu alifika mipakani mwa Uyahudi, na ng’ambo ya Yordani; makutano mengi wakakutanika tena wakamwendea; akawafundisha tena kama alivyozoea. Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamwuliza, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe? Huku wakimjaribu. Naye akajibu, akawaambia, Musa aliwaamuru nini? Wakasema, Musa alitoa ruhusa kuandika hata ya talaka na kumwacha. Yesu akawaambia, Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu aliwaandikia amri hii. Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja, hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe. Hata nyumbani tena wanafunzi wakamwuliza habari ya neno hilo. Akawaambia, Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake; na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini.
Maoni
Ingia utoe maoni