Ijumaa. 22 Novemba. 2024

Mt. Silvesta wa Kwanza, Papa

Silvesta wa Kwanza, Papa

Zipo hadithi mbalimbali kumhusu Papa huyu, lakini hizo hazina msingi wowote kihistiria. Hivyo Papa Silvesta wa Kwanza anajulikana zaidi kwa ajili ya mambo yaliyotukia wakati wa upapa wake kuliko kwa ajili ya yale aliyoyasema au kuyatenda yeye mwenyewe.

Alizaliwa mjini Roma (Italia) katika familia ya mtu Mroma aliyeitwa Rufino. Miaka kadhaa baada ya kupadirishwa na kupewa uaskofu, alichaguliwa kuwa Papa mnamo mwaka 314, mwaka mmoja tu baada ya yale mapatano ya Milano.

Tangu zamani, ilikuwa ni marafuku kuwa Mkristu katika Dola ya Roma, na kwa hiyo Wakristu wengi sana walidhulumiwa na hata kuuawa kwa ajili ya Imani yao kwa Yesu. Lakini miaka michache tu baada ya Konstantino kujipatia madaraka kama Kaisari wa Roma, alitoa sheria iliyowapa Wakristu uhuru wa dini. Sheria hiyo ilitolewa mwaka 313 nayo yajulikana kama mapatano ya Milano. Kwa hiyo basi, Silvesta alipochaguliwa kuwa Papa wa Kanisa zima, hali ya Kanisa ilikuwa tulivu sana. Mateso ya Wakristu yalikomeshwa mahali pote alipotawala Konstantino, Makanisa yalijengwa kwa gharama ya Serikali, siku ya Jumapili iliwekwa kuwa ya kupumzika kwa maofisa wa serikali, na kwa jumla Kanisa liliendelea kustawi mahali pengi. Ni katika wakati huu huu ndipo Kanisa la kwanza lilipojengwa kwenye mlima wa Vatikano mahali hapo alipokuwa amezikwa Mtakatifu Petro.

Jambo kuu lingine lililotukia wakati wa utawala wa Papa Silvesta wa Kwanza ni kuitishwa kwa Mtaguso Mkuu mjini Nikea (Uturuki) mwaka 325. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kabisa kwa wajumbe kutoka sehemu zote za Dola ya Roma kukutana mahali pamoja. Fundisho kuu lililotangazwa hapo ni kwamba Yesu ni Mwana wa Pekee wa Mungu Baba, mwenye hali moja na Baba; akiwa Mungu kweli na mtu kweli, walitangaza pia Bikira Maria ni Mama wa Yesu Kristu na Mama wa Mungu.

Papa Silvesta alifariki mwaka 335.

Maoni


Ingia utoe maoni