Ijumaa. 22 Novemba. 2024

Mt. Familia Takatifu

Familia Takatifu

Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, huadhimishwa kila mwaka siku ya Jumapili ifuatayo Sherehe ya Kuzaliwa Bwana, lakini sherehe hiyo inapoangukia siku ya Jumapili, basi, Sikukuu ya Familia Takatifu yaadhimishwa tarehe 30 Desemba.

Familia ya Maria, Yesu na Yosefu ilikuwa familia yenye dhiki. Mungu alipowaomba Yosefu na Maria kuwa baba na mama wa mtoto wa Kimungu, alikuwa amemwomba jambo gumu. Hata ile nafasi ya kumzalia mtoto Yesu ilikosekana kati ya watu. Na muda mfupi tu baada ya kuzaliwa, mtoto alitafutwa na askari wapate kumwua kwa amri ya Mfalme, na saa ya usiku wazee wake walilazimishwa kukimbia haraka haraka ili kumsalimisha mtoto wao. Siku ambayo Maria alikwenda Hekaluni, kwa fahari kubwa, kumtolea mzaliwa wake wa kwanza kwa Mungu, maneno ya mzee Simoni kwamba "Uchungu ulio kama upanga mkali utauchoma moyo wako", hakika, yalimshtusha sana hata kumwogopesha. Huzuni na hofu ya Yosefu na Maria ilikuwa kubwa sana siku ile walipotambua kuwa mtoto wao alikuwa amepotea, hata walipompata tena, wakaweza kumkemea: "Kwa nini umetutendea hivyo?" Ilikuwa sio rahisi kwa Yosefu na Maria kuubeba mzigo wa kuwa baba na mama wa mtoto Yesu. Lakini, hata hivyo, walifaulu kuitekeleza vizuri kazi waliyokuwa wamepewa na Mungu.

Walifauluje? Walifaulu kwa sababu maishani mwao waliyaweka mapenzi ya Mungu kama kiini cha utendaji wa kazi yao, hayo yakiwa ni upendo, yaani kupendana, kusameheana na kusaidiana. Kama wale wote waishio wakaao pamoja wangejitahidi kuiga mfano huo, basi, shida nyingi za maisha ya kuishi pamoja zingepungua na hata kutoweka kabisa.

Katika liturjia ya Ekaristi ya sikukuu hii, kanisa limechagua sehemu ya barua ya Paulo Mtume kwa watu wa Kolosai, kwamba "Vumilianeni na kusameheana iwapo mmoja wenu analo jambo lolote dhidi ya mwenzake". (Kol. 3:13) na katika sala ya siku hii twasali hivi: "Tuweze kufuata mifano ya hiyo Familia Takatifu katika fadhila za nyumbani na kuungana kwa mapendo".

Maoni


Ingia utoe maoni