Tomasi Beket
Toma Beket alizaliwa mjini London (Uingereza) mwaka 1118. Wazee wake ambao majina yao ni Gilbert na Matilda, walikuwa raia wa kawaida na watu wa dini kweli kweli. Akiwa na umri wa miaka ishirini na moja, Toma alifiwa na mamae, na baada ya muda mfupi babaye naye akafariki pia. Baadaye Toma alipewa kazi nyumbani mwa Teobaldi, askofu mkuu wa Kantabari (Uingereza). Kwa kuwa askofu huyo alimpenda Toma, alimsaidia ili afanikiwe katika njia yake ya kuwa padre. Basi, mwaka 1154 alipewa ushemasi.
Kadhalika, mfalme wa Uingereza, Henriko wa Pili, alimpenda sana Toma, na hivyo, kwa ajili ya uhusiano wake na Askofu Mkuu, pia na Mfalme, Shemasi Toma alipewa wadhifa mkubwa serikalini, hata akawahi kuwa waziri mkuu wa Uingereza. Kufuatana na hali hiyo, alipata watumishi wengi, akavaa kimaridadi, na kuhudhuria katika karamu nyingi sana. Kwa tabia yake Toma alikuwa mtu mwenye kiburi na mwepesi wa kukasirika. Hata hivyo, aliishi maisha ya sala, alifanya mafungo ya kiroho na hata kujiadhibu kwa kujipiga mijeledi. Mwaka 1161, askofu mkuu wa Kantabari, Teobaldi, alipofariki dunia Mfalme Henriko alimtaka Shemasi Toma kushika nafasi yake, lakini Toma alikataa kabisa akisema: "Wataka nikubali kuwa askofu, lakini nionavyo mimi, si sawa kwa maana itakuja siku tutakapokorofishana kuhusu haki za kanisa, nawe utanikasirikia". Lakini kwa kuwa Balozi wa Papa alimfanya aikubali hadhi hiyo, Toma akatii akapewa upadre mwaka 1162, na siku chache baadaye akasimikwa kuwa askofu. Ndipo namna yake ya kuishi ilipoanza kubadilika. Kwanza, alijiuzulu kuwa waziri mkuu; halafu, aliwaomba baadhi ya mapdre wenzake wamjulishe kinaganaga makosa watakayoyagundua kwake. Akazidi kufanya malipizi kwa namna mbali mbali na kutoa msaada wa fedha kwa watu wengi.
Siku moja Mfalme Henriko alitunga sheria zilizopingana na zile za kanisa, ambazo askofu Toma hakuweza kukubaliana nazo. Kwa hiyo, mfalme akaanza kumchukia sana rafiki yake wa zamani, ikampasa Askofu Toma kukimbilia Ufaransa, ambako alikaa kwa muda wa miaka saba.
Alipopewa ruhusa ya kurudi Uingereza, adui zake walianza kumchochea Mfalme dhidi ya Askofu Mkuu Toma. Na siku moja Mfalme Henriko alisema: "Lini nitaweza kumshinda askofu yule?" Neno hilo lilitosha kabisa. Watu wanne wakamwendea Askofu Mkuu, wakamkuta katika Kanisa lake Kuu, wakampiga upanga kichwani, wakamchoma visu na kuvunja fuu la kichwa hata ubongo ukamwagika chini mbele ya altare. Alipokuwa akitendewa hivyo, Askofu Mkuu Toma alimwambia: "Msiwadhuru Mapadre wangu"
Maoni
Ingia utoe maoni