Watoto Watakatifu
Leo, Kanisa lawakumbuka watoto ambao Mwinjili Matayo amewataja katika injili yake. Hao waliuawa kwa amri ya Mfalme Herode kwa sababu alimwangalia mtoto, mfalme wa Wayahudi aliyezaliwa, kuwa ni hatari katika ufalme wake. Huenda, siku moja, mtoto huyo angeweza kumnyang'anya ufalme wa Yudea. Kwa hiyo, ili asije akaupoteza ufalme wake, akawahi kuitoa amri ile mbaya.
Ni Mamajusi, wale wataalam wa nyota, waliokuja mjini Yerusalemu toka nchi ya Mashariki ili kumwabudu Bwana Yesu, ndiyo walioileta habari ya Yesu kuzaliwa. Kwa kuwa wataalam hao hawakuijua njia ya kwenda Betlehemu, walimwendea Mfalme Herode kuomba msaada, ili waelekezwe njia hiyo, lakini Herode alikuwa hana habari bado ya Yesu. Walimu wa Sheria walimweleza kwamba kijiji chenyewe ni Betlehemu. Basi, mfalme Herode aliwaomba Mamajusi waende kumwabudu yule mtoto, na baadaye wampe habari ya alipo Yesu, ili Herode naye aende kumtukuza. Lakini Mamajusi hao walionywa katika ndoto wasimrudie Herode. Kumbe, mfalme alipogundua kwamba wataalam wa nyota walikuwa wamemhadaa, ndipo alipotoa amri ya kuwaua watoto wote wa kiume mjini Betlehemu waliozaliwa tangu miaka miwili.
Mwinjili Matayo, akiandika habari hiyo, ameonyesha kwamba Herode hakumfahamu Yesu wala madhumuni ya kuzaliwa kwake: Yesu, kama alivyoeleza mwenyewe karibu na mwisho wa maisha yake, alikuwa hana haja ya ufalme wa dunia hii, bali alitaka kuitawala mioyo ya watu.
Sikukuu ya leo yatufikirisha kwamba hakuna mwanadamu awezaye kuubatilisha mpango wa Mungu. Zamani za kale, Farao wa Misri alijaribu kuutangua mpango wa Mungu alipoamuru watoto wote wa kiume wauawe, lakini hat hivyo, mmoja wao, yaani Musa, aliokolewa, akawa mwokozi wa Wayahudi na kiongozi wao. Yesu ni Mkuu kuliko Musa: Yeye ni Mwokozi na kiongozi wa wale wote wanaotaka kumfuata. Kama vile Farao wa Zamani, mfalme Herode naye alijaribu kumwondoa yule atakayeweza kuwa hatari kwake. Lakini, kama vile Musa wa zamani, Yesu aliokolewa kwa nguvu ya Mungu, akawa Mwokozi na Kiongozi.
Watoto watakatifu huheshimiwa kama wafiadini. Waliuawa kwa ajili ya Bwana Yesu; hawakumshuhudia kwa maneno yao, bali kwa mateso na kifo chao.
Maoni
Ingia utoe maoni