Yohani , Mtume na Mwinjili
Mt. Yohani alizaliwa Betsaida mkoani Galilaya (Israel). Baba yake alikuwa Zebedayo na mama yake alikuwa Salome. Alikuwa ndugu wa Mt. Yakobo, aliyashuhudia mambo makuu yaliyotukia maishani mwa Bwana. Hivyo, Bwana alipogeuka sura mlimani Tabor, na tena alipokuwa akisali bustanini Getsemane, Yohani alikuwapo. Aidha, Bwana alimponya mama mkwe wa Petro, vile vile alimfufua binti Yairo, mtume Yohani alikuwepo pamoja na Petro na Yakobo.
Yohani hujulikana kama mwanafunzi aliyempenda Yesu. Huyo ndiye yeye ambaye wakati wa karamu ya mwisho alikuwa ameketi karibu na Yesu, na baadaye, saa alipokuwa akifa Yesu, ni yeye tu kati ya Mitume wote aliyesimama karibu na msalaba pamoja na Bikira Maria, Maria wa Kleopa na Maria Magdalena.
Baada ya Yesu kufa msalabani, Yohani alimchukua Bikira Maria akae nyumbani kwake. Alipoletewa habari ya Bwana kufufuka, mara alikimbia pamoja na Petro; japo Yohani alikimbia upesi zaidi kuliko Petro na kutangulia kufika kaburini, alimsubiri Petro ili huyo apate kuwa wa kwanza kuingia ndani. Lakini Yohani ndiye aliyeanza kuamini kwamba amefufuka alipokiona kitambaa alichofungiwa Yesu kichwani, kimekunjwa na kuwekwa mahali pa peke yake.
Yohani aliishi akawa mzee sana. Wakati wa utawala wa Kaisari Domisian (tangu mwaka 81 hadi 96) alihamishwa kwa nguvu hadi kisiwa cha Patmos, na hapo ndipo alipokiandika kitabu cha UFUNUO. Katika maisha yake, Yohani alipata kudhulumiwa na kuteswa sana, bali kati ya Mitume wote ni yeye tu ambaye hakudiriki kuuawa. Aliandika barua tatu ambazo ni sehemu ya Kitabu cha Agano Jipya. Katika barua hizo, kama vile ilivyo katika Injili yenye jina lake, Yohani hasa ni mtangazaji wa uhai mpya wa neema ambao tumeletewa na Kristu.
Alivyoandika katika barua yake ya kwanza (1Yoh. 1:3), kazi yake kuu ilikuwa kukitangaza kile alichokiona na kukisikia yeye mwenyewe muda alipokuwa akishirikiana na Bwana Yesu. Aliyaandika yale yote ili watu wapate kushirikiana na Mitume katila umoja waliokuwa nao na Baba na Bwana Yesu. Kazi hiyo, Yohani aliitekeleza kwa furaha kubwa, kiasi cha kukamilisha furaha yake.
Katika ujana wake, yeye, Yohani, pamoja na ndugu yake Yakobo, walikuwa wakali kidogo kwa tabia, hata siku moja, walitaka kuamuru moto ushuke toka Mbinguni ili uwaunguze wenyeji wa kijiji kimoja cha Wasamaria, eti, kwa sababu walikataa kumpokea Yesu. Waliwahi kupewa na Yesu jina Boanerge, maana yake "Wanangurumo". Mahali pengine katika Injili imetajwa ile hamu ya ukuu waliyokuwa nayo hao ndugu wawili. Imeandikwa kwamba walimsukuma mama yao awaombee kwa Yesu ruhusa ya kuketi apo baadaye upande wake wa kushoto na kulia na wa kushoto. Sasa, kuna hadithi moja kumhusa Yohani, Mtume ambayo yafaa kuikumbuka kwa vile inavyoonyesha jinsi tabia yake ilivyobadilika. Yasemwa kwamba alipokuwa mzee, hakuweza tena kufundisha sana, lakini siku zote alikuwa akilikariri neno lile lile moja: "Wanangu, Mpendane". Hatimaye, wakristu walichoka kulisikia neno hilo, wakamnung'unikia na kumwuliza: "Je, hujui neno jingine ila hilo tu? " Naye akawajibu: "Neno hilo ni amri ya Bwana wetu; mkilifuata vema, basi yatosha".
Maoni
Ingia utoe maoni