Stefano
Wakristu walipoanza kuwa wengi, matatizo yalianza kuongezeka kutokana na ubaguzi wa kikabila. Kitabu cha Matendo ya Mitume chaelezea kwamba kulitokea manung'uniko kati ya waumini waliokuwa wakizungumza Kigiriki na wale waliozungumza Kiebrania. Wayahudi wa Kigiriki walinung'unika kwamba wajane wao walikuwa wanasahauliwa katika ugawaji wa mahitaji ya kila siku. Tukio hilo lilisababisha uteuzi wa mashemasi wa kwanza, ambao kati yao alikuwa Stefano ambaye mauaji yake yanakumbukwa mpaka hivi leo. Kama vile Mashemasi wenzake, alijawa na Roho Mtakatifu na kuwa mwenye hekima; zaidi ya hayo, Stefano alikuwa mtu aliyejaliwa neema tele, nguvu nyingi na uwezo wa kutenda miujiza na maajabu kati ya watu.
Wayahudi kutoka Kurene, Aleksandria, Kilikia na Asia walibishana naye juu ya mambo ya dini, lakini hawakuweza kumshinda. Mwishowe, wakawachochea watu, wazee wao na hata walimu wa sheria. Wakamkamata Stefano na kumleta mbele ya Baraza Kuu. Hapo walimshtaki kwa uongo kwamba mara nyingi alisema maneno ya kulikashifu Hekalu.
Stefano alijieleza kwa kirefu akiwaonesha jinsi, tangu zamani za kale, Waisraeli walivyomwasi Mungu mara kwa mara kwa kutowakubali viongozi aliowatuma kwao. Wote wa Baraza Kuu walimsikiliza kwa utulivu. Lakini Stefano alipoanza kuwashtaki kwamba walikuwa wakaidi na kumpinga Roho Mtakatifu; kwamba mioyo na masikio yao yalikuwa kama ya watu wa mataifa, yaani ya watu wasioteuliwa na Mungu, ndipo wazee wa Baraza Kuu walipoghadhibika sana. Stefano akaendelea kusema kwamba alikuwa ameona Mbingu zimefunguliwa, na Yesu, Mwana wa Mtu, amesimama upande wa kulia wa Mungu. Hapo wazee wakashindwa kuvumilia zaidi kwa sababu hawakutaka kukubali ya kwamba Yesu, aliyesulubiwa nao, alikuwa Mwana wa Mtu, hadhi ambayo maana yake ni Masiha. Basi, wakamrukia Stefano, wakamtoa nje ya mji na kumpiga mawe. Hivyo Stefano akawa mfuasi wa kwanza aliyeifia imani yake kwa Bwana Yesu. Kama vile alivyofanya Mwalimu wake, naye Stefano aliwasamehe wauaji wake, akiwaombea.
Miongoni mwa wale mashahidi alikuwepo kijana Paulo. Kutokana na maelezo ya Biblia, watu waliyaweka makoti yao chini ya ulinzi wake, naye mwenyewe alikiona kile kitendo cha kumwua Stefano kuwa ni sawa kabisa. Katika mapokeo ya Kanisa inasemekana ya kwamba Stefano, kulingana na mastahili yake, alimpata mdhalimu wake wa hapa duniani ili awe rafiki yake huko mbinguni; na ya kwamba Stefano alitangulia kwenda Mbinguni akiuawa kwa mawe ya Paulo, naye Paulo akamfuata huko akisaidiwa kwa maombezi ya Stefano
Maoni
Ingia utoe maoni