Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Mt. Anastasia

Anastasia

Habari zilizoandikwa juu ya Mtakatifu huyu zaonyesha jinsi pengine ilivyo vigumu kutofautisha kati ya mambo yaliyotukia kweli maishani mwake na habari zilizobuniwa tu. Jamboa pekee la Mt. Anastasia ni kwamba jina lake hutajwa katika sala ya Ekaristi ya kwanza iitwayo Sala ya Kiroma, nalo laweza kuangaliwa kama ishara ya kwamba Mtakatifu huyu ni mwenyeji wa Roma. Hata hivyo hakuna habari yoyote inayojulikana kwa hakika juu yake isipokuwa kwamba karne ya nne aliuawa mjini Sirmio (Yugoslavia) kwa ajili ya dini yake ya kikristu, wakati wa utawala wa Kaisari Dioklesiano.

Baadaye wenyeji wa Roma walipopata habari ya Mfiadini huyo, walianza kuona uhusiano na kanisa mojawapo lililokuwa limejengwa mjini mwao na mwanamke ambaye yeye naye aliitwa Anastasia. Japo kanisa hilo halikuhusiana hata kidogo na mfiadini Mtakatifu aliyeuawa mbali na Roma, hata hivyo likaanza kuitwa kanisa la Mt. Anastasia, ili kumhusisha kweli mfiadini mtakatifu jina lake likaanza kutajwa katika Sala ya Ekaristi ya Roma, na hadithi mbalimbali zikaanza kubuniwa. Labda sehemu ya hadithi ni mapokea yaliyosimuliwa toka vizazi na vizazi.

Hivyo inasemekana alizaliwa mjini Roma katika ukoo bora, akaolewa kwa nguvu na mpagani mwenye tabia mbaya. Anastasia alikuwa mkristu hodari, akawa na kawaida ya kuwatembelea kisirisiri wakristo waliofungwa mjini, kuwatibu vidonda, kuwaletea chakula na hata nguo. Kwa ajili ya hatari ya kukamatwa, alikatazwa na mumewe asitoke tena nje, baada ya kufiwa na mumewe, Anastasia akahama Roma ili kukaa karibu na kiongozi wake wa roho, Mtakatifu Krisogoni, mjini Akwileya, Italia ya Kaskazini. Hapo aliendelea na kawaida yake na kuwatembelea na kuwasaidia wakristu wafungwa. Na siku moja wakakamatwa.

Zipo tena hadithi kadhaa za mateso yake, lakini hakika ya historia haipo. Husemwa kwamba alipelekwa barazani, akahojiwa, akashurutishwa kutoa sadaka kwa sanamu, lakini akakataa kabisa. Kisha wakamshawishi kwa namna mbalimbali, lakini hawakufaulu kumfanya akubali. Basi, akafungwa kwenye chumba kidogo chenye uvundo na giza, peke yake kabisa, akapewa chakula kidogo sana. Baadaye alichomwa moto, mnamo siku ya Noeli mwaka 304.

Ibada yake ilienea sana, kwanza katika nchi yake mwenyewe, yaani Yugoslavia, na baadaye nchini Roma na hata nchi nyingine. Japo mengi sana tunayoambiwa juu ya Mtakatifu huyu ni hadithi tu, hata hivyo jambo kuu linabaki, palepale nalo ni kwamba aliishi kikristu kwa uhodari, wala hakuogopa kuvumilia maumivu ili kumdhihirishia Kristu upendo wake.

Maoni


Ingia utoe maoni