Jumapili. 24 Novemba. 2024

Mt. Yohani wa Kanti

Yohani wa Kanti

Yohani alizaliwa Kanti, jimboni Krakau (Poland) mwaka 1390. Kiisha kupadirishwa aliwekwa kuwa Mwalimu wa Chuo Kikuu, akafanya bidii kuwalea wanafunzi wake katika uchaji wa Mungu. Padre Yohani alifuata mfano wa Yesu Kristu Mchungaji Mwema, akatoa fedha yake yote kuwasaidia Wakristu maskini; na mwisho alikuwa akiwagawia viatu na mavazi yake. Alichukia mavazi ya kimalidadi, alifunga siku nyingi, na kujitesa sana. Alifanya ibada kuu ya mateso ya Bwana Wetu, na ndiyo maana alikwenda Yerusalemu kuhiji kwenye nchi Takatifu; safari hii ilimsaidia sana kwa mafundisho ya Biblia.

Mara nne alifunga safari kwenda Roma (Italia) kumheshimu papa, na kujipatia rehema ili azikomboe roho za toharani. Siku moja alipokuwa akisali njiani, wezi walimrukia na kumnyang'anya fedha zake na kumwuliza: "Una bado fedha nyingine?" Akawajibu: "Sina". Basi walimwachia aende zake. Lakini mara alikumbuka vilibaki vipande vingine vya dhahabu alivyoshononelea kwenye kanzu yake. Kwa kuogopa labda amesema uwongo, aliwakimbilia wanyang'anyi hao akwaambia: "Nimesahau dhahabu hii kuwapa". Akawapa. Wanyang'anyi wale walipoona unyofu wa Padre Yohani, waliona haya, walikiri kosa lao, wakamrudishia mali yake yote.

Yohani wa Kanti alikufa mjini Krakau mwaka 1473, na alitajwa Mtakatifu mwaka 1767. Sikukuu yake inaadhimishwa kwa heshima kubwa huko Poland.

Maoni


Ingia utoe maoni