Jumapili. 24 Novemba. 2024

Mt. Petro Kanisio

Petro Kanisio

Petro Kanisio alizaliwa na wazazi wakatoliki mjini Nymegen (Uholanzi) mwaka 1521. Alipokuwa na umri wa miaka mitano, alifiwa na mamae. Mama huyo alikuwa mkristu hodari na mwenye imani thabiti. Petro mwenyewe ametusimulia kwamba mara nyingi mamae alisali sana ili kumkabidhi mtoto wake kwa Mungu; na kabla hajafarikia dunia, alimfanya mumewe aahidi kwamba daima atajitahidi kuwalea kikatoliki watoto wake. Petro alipokuwa na umri wa miaka kumi na minne, alipelekwa Koloni (Ujerumani) kujifunza katika chuo kikuu na kupata shahada; kisha, akaenda Lovani (Ubelgiji) kusomea digrii katika sheria ya kanisa.

Aliamua kuwa mtawa akaingia shirika la Mayesuiti ambalo lilianzishwa wakati ule wa Mt. Inyasi (taz. 31 Julai). Petro alikiwa Mholanzi wa kwanza kuwa Myesuiti, na Inyasi mwenyewe ndiye alikuwa mwalimu wake.

Baaada ya kuweka nadhiri zake za kitawa na kupadirishwa, padre Petro aliagizwa kuwaongoza wanafunzi wa shirika lake. Akiwa katika harakati za kuutekeleza wajibu huu aliweka msingi na mpangilio wa kazi zote za kufundisha wanazozifanya Mayesuiti nchi Ujerumani. Kwa njia ya kazi hiyo, Mayesuiti walilea kundi la Walei ambao waliondokea kuwa viongozi wakatoliki hodari, na wengine wengi wakawa mapadre wenye ibada na elimu ya hali ya juu.

Baadaye Padre Petro alitumwa kushiriki katika mtaguso mkuu wa Trento uliofanyika ili kulirekebisha Kanisa baada ya fujo iliyosababishwa na Waprotestanti wa kwanza kama vile Luteri na Kalvini. Mtaguso huo ulifunguliwa mwaka 1545. Katika mikutano hiyo, padre Petro aliwaonyesha maaskofu jinsi maelezo ya Sakramenti na hasa ya Ekaristi yaliyotolewa na waprotestanti yalivyopingana na mafundisho ya kanisa ya tangu zamani.

Hivyo alikuwa mtu mwenye nguvu sana katika kuyahuisha maisha ya kikatoliki wakati ule, na kama wakazi walio wengi wa Ujerumani ya kusini waliendelea kubaki wakatoliki badala ya kuasi dini, jambo hilo linatokana na juhudi za padre Petro Kanisio. Lakini licha ya bidii zake hizo, padre Petro, tofauti na wateteaji wengi wa dini katoliki wa siku zile, yeye hakuwa na uhasama katika uhusiano wake na Waprotestanti, bali aliweza kuwaelewa kidugu.

Jitihada zake zilijidhihirisha hasa katika mahubiri na maandishi yake. Tangu ujana wake, alikuwa ameitambua nguvu ya vitabu vizuri juu ya wasomaji, akaanza kuviandika mwenyewe. Kati ya vitabu alivyovitunga yeye, 'Katekisimu' yake ilikuwa muhimu sana. Kitabu hicho kilihitajika mahali pengi sana kwa ajili ya maelezo yake wazi kwa dini katoliki, hata kikakusudiwa kuchapwa mara kwa mara, na matoleo mia tano yaliweza kutembezwa; aidha kilitafsiriwa kwa lugha nyingine ishirini na tano.

Zaidi ya hayo yote, padre Petro aliwahi kusafiri sana kwa sababu aliombwa kuhubiri mahali pengi, na msaada wake ulihitajiwa na watu wa nchi kadhaa. Alikuwa mtu mashuhuri sana katika uhai wake. Mt. Fransisko wa Sale (taz. 24 Januari) alimwandikia barua ya kwamba “Yote uliyoyahubiri, uliyoyaandika na kuyafanya vizuri sana kwa ajili ya Kristu, yamekufurahisha kati ya wote wampendao Kristu".

Kazi yake ya mwisho aliyopewa ilikuwa ni kuunda Chuo mjini Friburg (Uswisi) nayo ilimfanya akae huko miaka kumi na saba ya mwisho ya maisha yake. Alifia huko mwaka 1597. Mwaka 1925 alitajwa Mtakatifu na pia Mwalimu wa Kanisa kwa ajili ya vitabu vile vingi alivyoviandika ili kuieleza kwa ufasaha dini ya Katoliki.

Maoni


Ingia utoe maoni