Ijumaa. 21 Juni. 2024

Mt. Lucia Bikira na shahidi

Lucia Bikira na shahidi

Mtakatifu Lusia ni mmojawapo wa wafiadini na mabikira wanaojulikana sana toka zamani na ibada ya kumheshimu imeenea mahali pengi. Kwa bahati mbaya, habari ya maisha yake haijulikani hata kidogo ila tu kwamba aliuawa kwa ajili ya dini ya Kikristu huko Sirakusa (Ziwani Sisilia, Italia) wakati wa madhulumu yaliyoamriwa na Kaisari Dioklesiano.

Kwa ajili ya hamu ya kumjua zaidi, watu walianza kuyabuni mambo, wakatunga nyimbo na mashairi kwa heshima yake. Hivyo, husemwa kwamba Lusia aliamua kuishi kibikira, lakini wazee wake walimposa kwa mvulana aliyekuwa mpagani. Lusia alipoanza kuwagawia maskini mali zake zote, mchumba wake alikasirika mno kiasi kwamba alimshtaki Lusia kwa Mkuu wa mkoa kwamba alikuwa mkristu. Basi, Lusia alipelekwa mbele yake, na alipokataa kabisa kuzitolea sadaka sanamu, alihukumiwa akokotwe nyumbani kwa malaya. Lakini Lusia alikaa imara wala hakuna aliyeweza kumng'oa hapo alipokuwa akisimama. Ndipo mkuu wa mkoa akaamuru LusIa auawe kwa panga. Basi, koo lake likachomwa upanga, naye akafa.

Mt. Lusia aliheshimiwa sana mjini Roma, katika karne ya sita, na kwa hiyo jina lake liliandikwa katika sala ya Ekaristi ya Kwanza. Japo habari ya maisha yake haina msingi katika historia, hata hivyo, yale yaliyobuniwa yanatudhihirishia upendo mkubwa ambao mtu sharti awe nao akitaka kuwa mwaminifu kwa Bwana mpaka mwisho.

Maoni

edwin msekalile

mt,lussia utuombee

Isaac Mhanga

Nimebalikiwa sana na Mt. Lucia

Ingia utoe maoni