Fransiska Kabrini
Fransiska alizaliwa Italia mnamo mwaka 1850 kama kitinda mimba wa mama yake ambaye alizaa watoto kumi na watatu. Saa chache baada ya kuzaliwa kwake, kundi la njiwa weupe lilitua uani kwao ambapo baba alikuwa ameanika nafaka. Japo alijitahidi kuwafukuza, walirudi tena mara kwa mara. Hiyo ilieleweka kuwa ni ishara nzuri. Kwa kuwa baba yake baba yake alimtaka kuwa mwalimu, alipelekwa katika shule ya bweni iliyoendeshwa na masista. Baada ya kumaliza masomo yake, alifiwa mapema sana na wazazi wake wote wawili. Fransiska alikuwa na hamu ya kuwa mtawa na mmisionari pia, na kwa hiyo aliomba kujiunga na shirika la masista waliokuwa wamefundisha shuleni, lakini hao hawakumkubali kutokana na afya yake kuwa dhaifu. Alijaribu kuingia katika utawa mwingine, alikataliwa mara ya pili.
Basi, akaanza kushirikiana na paroko wake kufundisha dini, kuwatembelea wagonjwa, kuwasaidia watu maskini, na kwa muda mfupi alifundisha shuleni. Akaombwa kusaidia katika nyumba ya mayatima. Japo hakuvutiwa na kazi hiyo, akakubali kuifanya kwa majuma mawili, lakini akabaki hapa miezi sita, akisaidiana na walezi wengine. Fransiska alitazamiwa kubadili nyumba hii pamoja na walezi wake iwe shirika la kitawa, lakini kiongozi mkuu alimchukia Fransiska na kuupinga kila mpango wake. Hata hivyo, Fransiska aliendelea kushirikiana vizuri na walezi wengine saba, ambao hao nao walitaka kumtumikia Mungu katika nchi za mision. Mwaka 1877 hao wote waliweka nadhiri zao za kwanza za kitawa. Lakini askofu aliamua nyumba hii ya mayatima ifungwe, akamwambia Fransiska ajaribu kuunda shirika la wamisionari mahala pengine.
Fransiska akaenda pamoja na wenzake, wakakodisha nyumba iwe konventi ya kwanza ya shirika jipya nalo likaitwa Shirika la Masista Wamisionari wa Moyo Mtakitifu, ambao kazi yao kuu ilikuwa kuwalea kikristu wasichana, wakafungua shule kwa ajili yao. Majaribu na vishawishi vilijaa pande zote, lakini hata hivyo shirika lilikua upesi, na Fransiska akachaguliwa kuwa mama mkuu wa kwanza. Alipoenda Roma, mwaka 1887, ya kuomba rasmi ruhusa ya kuwapo kwa shirika lake, watu wengi walijaribu kushauri vingine. Lakini hakuwasikiliza. Akafungua nyumba mbili mjini Roma, moja ilikuwa shule kwa wasichana, nyingine ilikuwa nyumba ya watoto. Mwaka uliofuata, wakuu wa Kanisa walikubali shirika lake na Sista Fransiska akashauriwa na Papa mwenyewe kuwatuma masista waende Marekani, kufanya kazi ya kitume kati ya wahamiaji wa Kiitalia.
Sista Fransiska alienda mwenyewe, na mnamo tarehe 31 Machi 1889 akatelemkia New York ulio mji mkubwa sana, na wakati ule katika mji huo tu wahamiaji wa Kiitalia walikuwa hamsini elfu. Shida kubwa aliyoikabili mara moja, ilikuwa kwamba mwanamke mfadhili alikuwa amevunja ahadi yake ya kumtayarishia Sista Fransiska na wenzake nyumba. Hivyo watoto waliomngojea kwa wingi na huku nyumba na shule vikakosekana. Mwishowe nyumba nyingine ikapatikana, lakini ilikuwa katika hali mbaya kwa vile ilijaa chawa na viroboto. Askofu wa New York akamshauri arudi Italia, lakini Sista Fransiska akakataa kabisa.
Badala yake akamtafuta yule mwanamke mfadhili, wakasikilizana kabisa, na nyumba ya masista ikafunguliwa. Tangu siku ile Sista Fransiska alijitolea kabisa akijishughulisha kwa kila namna. Alifungua nyumba sitini na saba katika nchi za Ulaya na Amerika. Alipokufa, shirika lake lilikuwa na masista mia tano; watoto elfu tano hivi walikuwa wanafundishwa shule na nyumba za mayatima, na wagonjwa aliowatunza katika hospitali zake walikuwa laki moja. Alizikabili shida za kila namna, vishawishi na maumivu, daima alikuwa njiani, na hata hivyo, ilivyoonekana, hakuchoka kamwe. Ifahamike kwamba kushughulika kwake hakukuwa tu namna ya kuukabili mtazamo fulani aliokuwa nao kitabia, bali shughuli zake nyingi zilikuwa tunda la upendo wake mkubwa kwa heshima ya Mungu. Upendo wake kwa Bwana ulibubujika matendo, nayo aliyafanya katika muungano thabiti wa kiroho naye. Hivyo Sista Fransiska alikuwa daima kielelezo cha watawa wote wenye elekeo la utendaji mwingi.
Alikufa kwa ghafla tarehe 22 Desemba 1917 mwenye umri wa miaka sitini na saba. Alitangazwa Mtakatifu mwaka 1946, akiwa raia wa kwanza wa nchi ya Marekani kupewa heshima hiyo kuu. Yawezekana kutumia juu yake maneno ya Mtume Paulo kwa Timoteo kwamba " Navumilia kila kitu kwa ajili ya wateule wa Mungu ili wao pia wapate ukombozi upatikanao kwa njia ya Yesu Kristu, na ambao huleta utukufu Milele" (2 Tim. 2: 10)
Maoni
Ingia utoe maoni