Mwenyeheri Urbano wa Tano, Papa
Urbano alikuwa Mfaransa aliyezaliwa mwaka 1310, na alipobatizwa aliitwa jina lake Wiliam. Baada ya kuhitimu mafunzo ya teolojia katika Chuo Kikuu cha Paris (Ufaransa) alijiunga na shirika la Wabenediktini, akapewa upadre; kisha hapo akawa anafundisha; baadaye akawa abati wa monasteri ya shirika lake.
Ifahamike kwamba wakati ule, tangu mwaka 1304 hadi 1378, Mapapa walikuwa wanakaa mjini Avinyoni (Ufaransa) badala ya mjini Roma, kwa ajili ya machafuko mengi yaliyoenea kila mahali nchini Italia siku zile. Kwa ajili ya kufanya shughuli rasmi nchini Italia, na hasa mjini Roma, Mapapa walituma mara kwa mara wajumbe wao. Papa Inosenti wa Sita mara nyingi alimtuma abati Wiliam.
Alipofariki papa huyo mwaka 1362, Makadinali walimchagua Abati Wiliam kuwa Papa, naye akalichagua jina liwe Papa Urbano wa Tano. Mapapa waliomtangulia walikuwa wamekusudiwa mara nyingi kurudi Roma, lakini kila mara walizuiwa na watu wenye vyeo, kama mfalme wa Ufaransa na Waziri wake, hata na baadhi ya makadinali. Upande mwingine, machafuko mabaya ya nchini Italia yaliwaogopesha Mapapa wengine wasirudi Roma.
Papa Urbano aliwashtusha wote alipoamua kurudi. Hakujali ripoti mbaya juu ya hali ya kuharibika kwa usalama wa nchi ya Italia, wala hakuwajali wakuu wa serikali ya Ufaransa waliojaribu kumzuia, wala hakuwasikiliza Makardinali waliomshauri asiende, Papa Urbano alikuwa imara: Kurudi atarudi tu. Katika miji yote aliyoipitia, wakatoliki wengi walisongamana njiani kumwona Baba yao wakimshangilia: "Sifa kwa Yesu Kristu, Papa aishi miaka mingi!" Mjini Roma alifanyiwa shangwe kuu na wenyeji ambao walipamba zote kwa bendera za kila rangi. Baada ya shangwe kuisha, ndipo Papa alipotambua jinsi hali ya mji wa Roma ilivyokuwa mbaya. Makanisa mengi yalikuwa magofu tu, na wenyeji wengi walikuwa wamehama, hata mapadre walikuwa wamelegea katika maadili yao, na watu maskini walikuwa wengi mno. Lakini Papa Urbano, japo alihuzunika sana, hakukata tamaa, bali akaanza kazi mara.
Kwanza aliwashawishi wasiojiweza wenye njaa, halafu waliojiweza walipewa kazi ya kutengeneza Makanisa na nyumba, na hata kujenga makanisa mapya. Aliwafundisha na kuwahubiria mapadre na watawa wawe tena watu wenye nidhamu bora. Lakini mzigo ulikuwa mzito kwake, ukazidi kumshinda. Aliombwa apeleke msaada kwa wakristu wa Ulaya ya kusini-Mashariki waliokuwa wakisumbuliwa na waturuki Waislamu, lakini Papa alikuwa hana msaada wa kutoa kutokana na hali mbaya ya nchi ya Italia: kila mahali alishuhudia vita vidogo vidogo, hapa na pale udanganyifu na ghasia. Pia mfalme wa Ufaransa na yule wa Uingereza walichukiana sana badala ya kupatana na kushirikiana kufanya vita dhidi ya Waturuki hao. Matumaini yote aliyokuwa nayo Papa Urbano yakaanza kuvurugika, na afya yake kuharibika. Siku kwa siku aliyakabili magumu yake yote kwa uhodari kwa ajili ya Bwana wake ambaye alitaka kuwa mtumishi wake mwaminifu. Lakini mwishowe hakuweza kuendelea zaidi.
Akiwa na huzuni moyoni mwake, aliamua kuondoka Roma, akarudi Ufaransa. Miezi mitatu naadaye akafariki dunia, mnamo tarehe 19 Desemba 1370. Inavyoelekea, Papa Urbano alishindwa kabisa, lakini hivyo sivyo. Bidii zake kubwa zililifanya Kanisa liwe na tumaini kubwa wakati ule uliokuwa mgumu sana kidini, kijamii na kisiasa. Kwa ajili ya bidii hizo aliitwa wakati ule 'Nuru ya Ulimwengu na Mpenda Maadili'.
Maoni
Ingia utoe maoni