Winibaldi, Abati
Winibaldi pamoja na mdogo wake Wilibaldi alitoka Uingereza kwenda Roma (Italia) kuhiji. Kwa kuwa aliugua huko, mdogo wake aliendelea peke yake hadi Nchi Takatifu, na Winibaldi alibaki Roma ambapo alianza kujifunza teolojia na Biblia kwa muda wa miaka saba, ndipo aliporudi nyumbani Uingereza ambapo alifanikiwa kuwavuta vijana wengine wajiunge naye, na pamoja nao akarudi Roma tena, akaingia utawa wa Mtakatifu Benedikto katika Monasteri ya Monte Kasino.
Mt. Bonifasi aliyekuwa Mwingereza na mmisionari nchini Ujerumani (tazama 5 Juni) alipofika Roma kumtembelea Papa, alimkuta Winibaldi katika monasteri ya Monte Kasino, akamwomba afuatane naye, yeye naye awe mmisionari kule. Ifahamike kwamba mdogo wake Winibaldi aliwahi kupadirishwa, akawa mmisionari nchini Ujerumani, akawa askofu huko. Pia kwamba dada yao Walburga, yeye naye alikuwa ametoka Uingereza, akawa mtawa nchini u Ujerumani (taz. 25 Februari). Basi, Winibaldi akakubali, na wote wawili, Bonifasi na Winibaldi, wakaelekea Ujerumani.
Huko Winibaldi alikabidhiwa Parokia saba, kila moja yenye eneo kubwa. Kazi hiyo ilikuwa ngumu kiasi cha kutosha, hasa kwa kuwa wapagani wa makabila mengine mara kwa mara waliishambulia kazi yake wakibomoa makanisa na kuwaua wakristu. Hata hivyo, aliendelea na kazi yake kwa moyo wote, Ndipo ndugu yake alimwomba amsaidie kujenga monasteri kwa ajili ya wanaume, na alimwomba dada yake amsaidie kuanzisha monasteri kwa ajili ya masista.
Ndivyo alivyofanya Mtakatifu Winibaldi. Monasteri yake ilikuwa ya Wamonaki Wabenektini, na akiwa abati aliendelea na safari za kitume ili kuwahubiria watu wengi Habari Njema ya Bwana Wetu. Jambo alilofundisha kwa umakini lilikuwa udumivu katika sala. Kwa ajili ya bidii zake dhabiti za kufanya watu waishi Kikristu, wawe na maadili mazuri, na kuachana kabisa na kila zoea lenye kushindana na amri za Mungu, abati Winibaldi, zaidi ya mara moja, alikabiliwa na kifo kutoka kwa wapagani waliotaka kumwua kwa sababu waliona alikuwa anabadili mazoea na mila zao. Japo afya yake ilikuwa si nzuri sana, hata hivyo aliendelea kujitoa bila kujihurumia wala kulegea, na hivyo nguvu yake juu ya watu wengi ilienea mahali pengi. Alikuwa mmisionari hodari ambaye nuru yake iling'ara wazi sana mbele ya watu wa Ujerumani ili wao nao wamjue na kumtukuza Baba Mungu.
Mwishowe alidhoofika sana, na alikuwa mgonjwa kwa muda wa miaka mitatu. Ndipo alipofariki dunia, mnamo tarehe 18 Desemba 761, wakiwapo dada yake na kaka yake.
Maoni
Ingia utoe maoni