Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Mt. Maria Rosa

Maria Rosa

Mtakatifu anayekumbukwa leo hii, alidhihirisha maishani mwake kiasi kikubwa sana cha upendo wakidugu kwa wagonjwa, watu maskini na wakiwa ambao alijitolea kabisa kwa ajili yao. Hiyo ilikuwa njia yake ya kuyatekeleza maneno ya Bwana: "Umpende mwenzake kama nafsi yako".

Wazazi wake walikuwa watu matajiri kwa kuwa baba yake alikuwa na viwanda vya nguo. Mama yake alizaa watoto tisa, na yule wa sita aliyezaliwa mwaka 1813, aliitwa Paula siku aliyobatizwa. Huyo alipofikia umri wa miaka kumi na saba, aliacha shule apate kufanya kazi za nyumbani baada ya mama kufariki dunia. Baba aliyetaka kumwoza binti yake, alifaulu kufanya mapatano mazuri, lakini Paula alimweleza nia yake ya kuishi kiseja, baba hakumpinga.

Kwa muda wa miaka kumi alikaa nyumbani akijishughulisha kutenda mema mengi ya kijamii na kuwasaidia kiroho wale walioajiriwa viwandani mwa babae. Hivyo alianzisha chama cha akina mama na kukusanya watu mara kwa mara kwa mafungo ya kiroho. Ugonjwa wa kipindupindu ulipozuka na kuwashika watu wengi kwa pamoja, katika mwaka 1836, Paula na mjane fulani walishirikiana kujichosha kabisa, wakiwatunza kwa upole na upendo mwingi wagonjwa wenye kuteseka sana.

Baadaye Paula aliombwa kuisimamia nyumba kwa ajili ya wasichana maskini sana, walioachwa kabisa na ndugu zao. Hiyo ilikuwa kazi aliyoipendelea kweli, na kwa muda wa miaka miwili alifanya kazi hii kwa moyo wake wote. Lakini aliiacha kwa ghafla alipoambiwa kwamba wadhamini hawakuwataka wasichana hao kulala nyumbani humo saa za usiku. Maana yake ilikuwa kwamba wasichana watunzwe saa za mchana, na za usiku wazurure tu mitaani. Paula alishindwa kabisa kuuelewa mpango wa namna hii, na kwa hiyo aliacha kazi. Muda mfupi tu ulipita, na, kumbe, Paula mwenyewe aliweza kuwafungulia nyumba wasichana kumi na wawili, na kuwaruhusu kulala humo humo saa za usiku. Japo afya yake ilikuwa si nzuri, lakini alikuwa mtu mwenye akili, uwezo wa kukumbuka mambo mengi, roho shupavu sana, na, zaidi ya yote, kipaji cha kusimamia kazi, na cha kuwaelewesha watu.

Mwaka 1840, alikusanya kundi la akina mama kwa kuwasaidia wagonjwa wa hospitalini. Nalo likawa shirika la kitawa. Masista hao hawakukusudiwa kuwa wauguzi tu, bali walitakiwa kutumia muda wao wote, na kujitoa moyo wao wote, katika kuwatunza wenye kuteseka, na kupunguza maumivu yao ya kimwili na vilevile yale ya kiroho. Shirika liliitwa Watumishi wa Upendo, na haraka sana kundi dogo la awali likawa na watawa thelathini na wawili, katika shirika hili Paula akaitwa jina lake Maria Rosa.

Licha ya kusababisha wivu na fikra mbaya, kazi yao ilisifiwa pande zote, na upesi sana masista waliombwa kutoa huduma katika hospitali ya pili. Shirika lilikubaliwa rasmi na Wakuu wa Kanisa, Roma, mwaka 1852, na miaka mitatu badaye Sista Maria Rosa alifariki dunia. Mwaka 1954 alitangazwa Mtakatifu.

Ipo hadithi isemayo siku moja wakati wa vita kundi la askari wenye mwendo potovu, walijaribu kuingia hospitalini kwa nguvu. Sista Maria alipoambiwa hivyo, akachukua msalaba mkubwa, na, pamoja na masista wawili wenye kubeba mishumaa iwakayo, akawakaribia askari. Hao askari wakauonea aibu mwendo wao, wakaondoka bila ya kusema neno. Msalaba huo upo bado mpaka leo, na unaheshimiwa sana na kila mgonjwa.

Maoni


Ingia utoe maoni