Adelaida wa Burgondia
Maisha ya mwanamke huyu Mtakatifu yanatushangaza kwa kadiri yanavyotudhihirishia kwamba hata watu wenye vyeo bora huwa na matatizo yao makubwa, na ya kwamba pengine maisha yao ni magumu kutokana na kutendewa vibaya na ndugu zao. Adelaida alizaliwa mwaka 931 kama mtoto wa mfalme wa nchi ya Burgondia ambayo siku hizi ni sehemu ya Ufaransa. Kadri ya mila za wafalme wa siku zile, aliposwa na wazee wake mapema sana, yaani miaka miwili tu baada ya kuzaliwa. Kutokana na maafikiano hayo aliolewa mwenye umri wa miaka kumi na sita na mfalme wa Italia. Lakini bahati mbaya zilianza kumwandama mapema sana.
Kwa ufupi zilikuwa hizi. Haujapita muda mrefu baada ya kuolewa Adelaida alifiwa na mumewe, na -ajabu-akafungwa ngomeni na mfalme mpya. Miaka mitatu baadaye aliokolewa na mfalme wa Ujerumani ambaye aliitwa jina lake Otto. Mfalme huyo alikuwa mgane mwenye mtoto mmoja. Alimwoa Adelaida ambaye alikuwa na umri wa miaka ishirini tu, na Adelaida alimzalia watoto watano. Japo uhusiano na mtoto wa kambo ulikuwa mgumu, hata hivyo, miaka hii ilikuwa ya heri na alipendwa sana na raia zake. Heri hiyo ilikoma ghafla, mume wake alipokufa, na mfalme mpya, yule mtoto wa kambo, alimlazimisha kuondoka ikulu kwa ajili ya uhusiano wao mbaya. Baada ya muda mrefu kidogo hao wawili walipatana na hali yao ikawa nzuri. Lakini haikudumu kwa sababu mfalme, yaani mtoto wake wa kambo, alifariki dunia. Mke wake aliposhika utawala wa nchi, huyo hakutaka kumwona mama mkwe karibu naye, na hivyo Adelaida alilazimika mara ya pili kwenda mbali, Malkia huyo akafa ghafla, na ndipo Adelaida alipoweza kurudi Ikulu, na mwenye umri wa miaka sitini sasa akakabidhiwa kazi iliyomzidi nguvu na tabia yake ile ya upole. Hata hivyo, alijitahidi sana akifanya yote aliyoweza kwa ajili ya raia zake kwa kadiri ya vipaji vyake.
Kwa upande wa dini alijengesha nyumba nyingi kwa ajili ya wamonaki na watawa, na hasa aliwasihi maaskofu kujaribu kuwafundisha na kuwaongoa wapangaji waliokaa mipakani mwa mashariki ya Ujerumani, na mara kwa mara waliokuwa wakihatarisha amani. Shughuli zake nyingi zilimdhoofisha sana, mbali ya yale magumu mengi aliyokuwa ameyavumilia maishani mwake; akafa mnamo 16 Desemba mwaka 999, mweye umri wa miaka sitini na nane.
Adelaida akiishi katika mazingira ya Ikulu ya mfalme, aliulinda daima moyo wake wa kidini. Ni moyo huo uliomfanya avumilie kishujaa magumu mengi toka kwa ndugu zake na maumivu yake mengine. Upendo wake kwa Bwana ulionekana katika bidii zake za kuwapenda watu. Hivyo, licha ya maumivu yake mengi, alibaki kuwa mtu mwema na mpole na kupendwa sana na watu ambao waliiona kwake mifano mingi ya upendo wa kidugu.
Maoni
Ingia utoe maoni