Jumamosi. 04 Mei. 2024

Mt. Mwenyeheri Antoni Grassi

Mwenyeheri Antoni Grassi

Mwenyeheri Antoni Grassi, Padre (1671)
Baada ya kuzaliwa nchini Italia mwaka 1592, akawa kijana mwenye akili na moyo wa ibada. Alipokuwa na umri wa miaka kumi na saba, alijiunga na shirika la Wa-Oratori lililokuwa limeanzishwa na Mt. Filipo Neri (taz. 20 Mei), akapadirishwa.

Siku moja wakati wa mvua alipigwa na umeme, na mshtuko alioupata ulikuwa mkubwa kiasi kwamba watu walikuwa na hakika ya kwamba atakufa tu, lakini akapona. Katika hali hii Antoni alitambua kwamba saa tunalodhani tunakufa, hatujali tena mambo ya dunia hii kwa kuwa twaona wazi hayana thamani. Kama padre, shughuli yake kubwa ilikuwa kuungamisha. Alijaliwa karama ya kuweza kuona hali ya dhamiri ya wenye kuungama. Mara nyingi aliwashangaza kwa kutaja dhambi walizokuwa wamesahau kuziungama au kutozitaja kwa ajili ya haya.

Kama mkuu wa jumuiya alijionyesha mwema na mpole, na kila mara alijitahidi kutafuta lililokuwa jema na la kupendeza kati ya wenzake. Alipoulizwa kwa nini hakuwa kidogo mkali zaidi, akajibu: "Nionavyo, sijui jinsi ya kuwa hivyo". Kufanya mazoezi magumu ya kujinyima ilikuwa si desturi yake wala hakuwashauri wengine kuyafanya. Alisema kwamba kunyenyekea akilini ni jambo la maana zaidi kuliko kusikia maumivu mwilini. Utii lilikuwa jambo muhimu kwake, na kwa hiyo alisisitiza kuishika kinaganaga kabisa katiba ya shirika lake. Mfano wa utii huo alioutoa, uliwapa wengine moyo wa kuuiga mfano wake. Kwa ajili ya mwenendo wake aliheshimiwa sana hata nje ya jumuiya zake, akombwa kusaidia mjini kuwapatanisha watu wenye kugombana, pia katika ghasia za kijamii. Hakukubali kuwatembelea watu kwa kufuata urafiki au sababu ya adabu njema, bali saa yoyote ile ya mchana na ya usiku alikuwa radhi kwenda kwa wagonjwa na maskini.

Inasemekana kwamba aliweza kutabiri mambo ya baadaye, na aliitumia karama hii kwa kuonya na kutuliza. Alifariki dunia mwezi Novemba mwaka 1671. Fadhila zake kuu zilikuwa uaminifu kwa katiba ya shirika lake, na upole alipokuwa mkuu wa jumuiya.

Maoni


Ingia utoe maoni