Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Mt. Yohana wa Msalaba

Yohana wa Msalaba

Mtakatifu Yohani wa Msalaba alizaliwa Fontiveri (Hispania) yapata mwaka 1542. Mama yake alimfunza tangu utoto wake kumpenda Bikira Maria. Alipopata umri wa miaka ishirini akaingia Shirika la Wakarmeli. Tangu mwanzo alijitesa vikali, chumba chake kilikuwa kama kaburi, na alivaa kiunoni mnyororo uliotiwa misumari yenye kuchoma.

Alijishughulisha sana pamoja na Mt. Teresia wa Avila (taz. 15 Oct) kujaribu kuwarudisha Wakarmeli katika kanuni zao za zamani, kazi ambayo ilimtoa jasho na kumtia katika majaribu mengi. Kwa sababu hiyo alichukiwa, hata wote wawili walitiwa msukosuko, na baadaye alitiwa gerezani kama mtoro na mkana dini. Lakini Mungu hakumwacha mtumwa wake, alimtoa nje ya gereza kwa miujiza. Baada ya kutoka tu gerezani, akaanza mara nyingine kazi yake ya kuwarudisha Wakarmeli katika sheria zao za hapo mwanzo kabisa, na akafaulu.

Siku moja alipokuwa akisali mbele ya msalaba, alisikia sauti ikisema: "Unataka tuzo gani kwa kazi ulizozifanya na kwa mateso unayovumilia?" Yeye akajibu: "Tuzo ninaloomba ndio kuteswa na kudharauliwa kwa ajili yako". Na kweli Mungu alimwacha atendewe alivyoomba; kwani baadaye aliondolewa katika usimamizi wa shirika lake la watawa. Aliandika vitabu vyenye mafundisho ya kiroho. Baadaye alipata vidonda vitano mguuni, ilibidi waukate ule mguu. Matibabu walipokuwa wakisitasita, Yohani aliwaambia: "Msiogope, ukateni tu ni tayari kuufuata utashi wa Bwana wetu Yesu Kristu". Baada ya kupokea Sakramenti za Wagonjwa alikufa mwenye kicheko cha furaha usoni pake huko Ubeda Mkoani Andalusia (Hispania), mwaka 1591. Alitajwa Mtakatifu mwaka 1726, na mwalimu wa kanisa mwaka 1926.

Maoni


Ingia utoe maoni