Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Mt. Yohana Fransiska wa Shantal

Yohana Fransiska wa Shantal

Yohani Fransiska alizaliwa huko Dijon (Ufaransa), mwaka 1572, katika ukoo uliosifiwa kwa umaarufu wake. Baba yake alikuwa mwekiti wa baraza kuu la Burgonye. Mama yake alikufa yeye alipokuwa bado mtoto mdogo.

Tangu utoto wake Yohana hakuweza kuwavumilia wafitini wasiofuata dini ya kweli. Siku moja alimsikia Mprotestanti akisema kuwa Bwana wetu Yesu Kristu hayumo katika Sakramenti ya Ekaristi. Yohana, ingawa alikuwa mtoto, alikasirika sana, akaungama bila woga ukweli wa mafundisho ya Kanisa Katoliki. Mprotestanti huyo alijaribu kumtuliza kwa kumpa halua. Lakini Yohana alizitwaa hizo halua akazitupa motoni akisema: "Hivi ndivyo watawaka wafitini wa dini wanaokataa kusadiki maneno ya Bwana wetu".

Yohana alipofikia makamo, walitaka kumwoza kwa Mprotestanti. Yohana alikataa akisema: "Afadhali kufungwa na kulalamika gerezani kuliko kuolewa na mfitini wa dini". Mwisho alifunga ndoa na bwana mmoja mkatoliki, jina lake Shantal. Yohana alijaaliwa na Mungu akazaa watoto wanne. Aliwalea katika uchaji wa neno la Mungu. Alisimamia nyumba yake kama inavyompasa mwanamke mkatoliki na mtakatifu.

Siku moja mume wake alikwenda kuwinda wanyama pamoja na wenzake. Huko alipigwa risasi na baada ya siku mbili akafa. Yohana aliona uchungu mkubwa sana, lakini alimsamehe yule mtu aliyemwua mumewe kwa bahati mbaya, na aliweka nadhiri ya usafi wa moyo mpaka kufa.

Aliandika jina la Yesu kifuani mwake kwa chuma cha moto, na akamchagua Mt.Fransisko wa Sales, askofu wa Geneva (tazama 24 Januari), awe mwungamishi wake. Hakukawia kuendelea sana katika utakatifu. Kwa shauri la Mt. Fransisko aliiacha dunia, ingawa watoto wake mwenyewe walimzuia asiende. Alikubali kusimamia shirika la watawa wa Watembeleaji, na alilieneza katika nchi mbalimbali. Alikufa kwa nguvu ya mapendo aliyompendea Bwana wetu Yesu Kristu; ilikuwa mwaka 1641. Alitajwa Mtakatifu mwaka 1767.

Maoni


Ingia utoe maoni