Alhamisi. 28 Machi. 2024

Mt. Fransisko Ksaveri

Fransisko Ksaveri

Fransisko Ksaveri alizaliwa Hispania mwaka 1506 na uzazi wa ukoo bora. Kama angalitaka angaliweza kujipatia ukuu mbele za watu, lakini siku moja, alipokuwa akisoma huko Paris (Ufaransa), Mt. Inyasi wa Loyola (tazama 31 Julai) alimwambia: "Ksaveri, yafaa nini kwa mtu kupata ulimwengu wote, akipoteza roho yake?" Baada ya siku za mafungo, Ksaveri na Mt. Inyasi, pamoja na wenzake Wayesuiti, wakafunga nadhiri ya kwenda katika nchi takatifu ili kuwatunza wakristu waliokuwa wakilalama utumwani wa Waislamu. Kwa kuwa hawakufaulu kwenda huko, badala yake walikwenda Roma (Italia), wakaonane na Papa ili afanye nao jinsi apendavyo. Pale Italia, Ksaveri alipewa upadre mwaka 1537. Mwaka 1540, Inyasi na Ksaveri walikuwa Roma kwa kupewa kibali rasmi cha shirika lao jipya.

Zamani hizo, Mfalme wa Ureno alimwomba Mt. Inyasi apeleke mapadre wa shirika lake kuhubiri Injili katika India. Fransisko Ksaveri akatumwa kwenda huko, pamoja na mapadre wengine wawili, katika mwaka 1541. Alijipakia merikebuni katika bandari ya Lisbon (Ureno), akavuka bahari na kushuka baada ya miezi kumi na mitatu, katika Pwani ya Goa (India). Huko Fransisko alizungukia nchi yote, akikusanya watoto na watumwa ili waje kufundishwa naye katekisimu, akisaidiwa na mkalimani. Watu wengi hawakukawia kuongoka. Miaka miwili baadaye, alihamia sehemu ya kusini ya India akiwafundisha, hasa wavuvi wa Pwani na visiwani, dini ya Yesu Kristu. Alitenda miujiza mingi, hata aliwafufua watu wanne. Watu wengi walipoona mwujiza huo walitaka kubatizwa.

Baada ya kuwapatia wenyeji wa huko mapadre, alisafiri katika Ufalme wa Trevankor (Sri lanka) na Indonesia, akafundisha dini katika visiwa vya Moluk, Amboina na Ternate akapata wakristu wapya wengi. Alitengeneza katekisimu ndogo katika lugha ya Ki-Malayan. Mwaka 1549 alishuka katika Pwani ya Japan ambamo alikaa kwa muda wa miaka miwili. Makasisi wao waliongea kwa mfalme, na hatimaye wakamfukuza katika nchi yao. Alirudi Goa, lakini hakukaa sana, lakini alitamani kupeleka injili katika nchi ya China.

Alipofika kisiwana Sanchian akaugua, wakamwacha huko. Mreno mmoja alimhurumia akampeleka kibandani mwake. Alikufa tarehe 2 Desemba mwaka 1552 katika kisiwa cha Sanchian huko China. Katika muda wa miaka kumi mmisionari huyu aliwabatiza watu wengi ajabu. Miezi miwili na nusu baada ya kufa kwake, waliukuta mwili wake haujaoza bado, ingawa alizikwa katika chokaa isiyozimka kusudi upate kuteketea upesi, ukapelekwa kwa heshima kubwa huko Goa (India), ambako umehifadhiwa hadi hii leo.

Ni rahisi kuzitaja na kuziorodhesha nchi alizokuwa amefanya kazi, bali sio rahisi sana kupata picha halisi ya uzito wa shughuli zile nyingi alizozifanya wakati wa miaka ile kumi na mmoja tangu aondoke Ulaya. Mbali na safari mbili za kwenda Japan na kwenda India, na baadaye kuvuka bahari kuelekea kisiwa cha Sanchian, alizifanya safari zake zote kwa miguu, akitembea kilometa nyingi, katika hali ya uchovu, ugonjwa, ugumu wa kazi, na kadhalika. Kweli, Mt. Fransisko alikuwa ni mtu hodari sana aliyesukumwa na upendo wake kwa Bwana ili utawala wake uzidi kuenea mioyoni mwa watu, na watu wengi zaidi wapate kumpenda na kumtumikia.

Katika barua mojawapo aliyomwandikia mkuu wake Mt. Inyasi, alisema: "Tangu nifike hapa, sijapumzika. Nimekitembelea kila kijiji, nikawaosha watoto wote wasiobatizwa bado kwa maji matakatifu. Hivyo kuna idadi kubwa sana ya watoto niliwaondolea dhambi ya asili. Watoto hawaniachii nafasi ya kusali breviari, kula na kulala usingizi kabla ya kuwafundisha walau sala fulani. Hapo nimepata kung'amua kwamba "Ufalme wa mbinguni ni kwa ajili yao"

Mtakatifu Fransisko Ksaveri alitajwa Mtakatifu mwaka 1622, na mwaka 1627 aliwekwa kuwa mlinzi wa wamisionari popote duniani. Siku ya leo yafaa sana kuwaombea, kwa Mtakatifu Fransisko Ksaveri, wale wote wenye kujitahidi kulitangaza kwa namna yoyote ili neno la Mungu.

Maoni

Frolentina Merdad

Somo wa jumuia yangu alimtafta mungu kwanguvu na akili zake zote yatupasa kufuata nyendo zake

Frolentina Merdad

Amina

edwin msekalile

aminaa,huo ndio utumwa

Ingia utoe maoni