Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Mt. Olimpia

Olimpia

Akiwa mtoto bado, Olimpia alifiwa na wazee wake wenye cheo kikuu, akalelewa na mwanamke mwadilifu na mwenye busara. Kwa sababu alirithi mali nyingi ya wazee wake, alikuwa msichana tajiri. Zaidi ya hayo, kwa ajili ya tabia yake na umbo lake alipendeza sana. Mt. Gregori wa Nazianze (tazama 2 Januari) alimwita "Kielelezo cha Wema". Ilikuwa rahisi kumwongoza bado akiwa kijana. Mume wake alikuwa mkuu wa mkoa, lakini kwa tabia alikuwa mtu mgumu. Huenda ilikuwa bahati kwa Olimpia kwamba kabla ya majuma matatu hayajapita baada ya kuolewa naye, na yeye akafariki. Ni dhahiri kwamba kiasi cha watu wengi wenye vyeo walimtafuta kwa kuwa walipenda kumwoa, hata Kaisari mwenyewe alimshawishi sana akubali kuolewa na ndugu yake, lakini Olimpia aliwakataa wote.

Kaisari aliamua Olimpia awekwe mikononi mwa mlezi rasmi, na kwa kazi hiyo alimchagua mkuu wa mji Konstantinopoli (Uturuki); huyo alilazimika pia kuisimamia mali ya Olimpia mpaka mwenyewe afikie umri wa miaka thelathini. Mlezi huyo alimzuia Olimpia asiende kanisani wala asiende kuonana na askofu mkuu wa mji huo. Basi, Olimpia akamwandikia barua Kaisari kuhusu mali zake, akamshukuru kwa kuwa alimwondolea mzigo wa kuisimamia; akatoa wazo ya kwamba afadhali aigawe mali hiyo kwa watu maskini. Ndipo Kaisari alipomrudishia Olimpia usimamizi wa mali yake.

Aliporuhusiwa kujitegemea tena, aliamua kuishi maisha ya sala na matendo mema, na kuitumia mali yake kwa kuirahisisha hali mbaya ya watu maskini. Askofu mkuu wa Konstantinopoli alimstahi sana, hata akamfanya kuwa shemasi wa kanisa lake. Alimpa nafasi katika nyumba ya wanawake wenye nia ya kujitoa kumtumikia Mungu. Hapa Olimpia alishirikiana nao kushona, kutengeneza na kufua nguo zote za kanisa.

Baadaye, Mtakatifu Yohani Krisostomo (tazama 13 Septemba) aliwekwa askofu mkuu wa Konstantinopoli, yeye naye alimheshimu sana Olimpia. Alipotambua kwamba Olimpia alikuwa mkarimu sana katika kuitumia mali yake, alimshauri awe na busara zaidi, kwa kuwa baadhi ya watu maskini walikuwa radhi kumtegemea walau kidogo, hata hivyo kubadili hali yao kiuchumi.

Askofu Krisostomo alipofukuzwa nchi ya Kaisari, Olimpia na wale wanawake wengine walianza kuteswa kwa ajili ya uhusiano wao naye. Olimpia alikamatwa, akashtakiwa kwa uongo kwamba alizichoma moto nyumba za serikali, akahukumiwa na kufukuzwa nchini. Wale wanawali wengine walisengenywa vibaya na kudhulumiwa. Askofu Krisostomo alimwandikia barua Olimpia ili kumtuliza na kumpa moyo. Barua kumi na saba zingalizipo bado mpaka hivi leo zilizoandikwa naye akimpelekea Olimpia, nazo ndizo zinazotupa habari juu ya mwanamke huyo Mtakatifu. Katika barua yake moja Askofu Yohani Krisostomo aliandika: "Sina budi kukuita mwenye heri".

Olimpia alifariki dunia mwaka 408 akiwa na umri wa miaka arobaini tu. Aliheshimiwa sana katika nchi za Ugiriki na nchi nyingine za Mashariki ya Kati, hata wasichana wengi sana walipewa jina la 'Olimpia'. Maisha yake yote yaweza kujumlishwa kwa aya ya Injili isemayo: "Msijiwekee hazina hapa duniani, bali jiwekeeni hazina Mbinguni ambapo nondo au kutu hawawezi kuiharibu" (Mt. 6:19-20).

Maoni


Ingia utoe maoni