Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Mt. Petro Furiye

Petro Furiye

Mtakatifu huyu ni Mfaransa aliyezaliwa mwaka 1565. Alielimishwa hadi chuo kikuu, na baada ya kuhitimu masomo yake vizuri sana, alianza mwenyewe kufundisha. Lakini maisha ya kitawa yalimvuta. Basi, akajiunga na watawa wa Mtakatifu Augustino, na miaka minne baadaye, alipewa upadre. Kwa kuwa alijiona hastahili kuwa padre, aliahirisha kuiadhimisha misa yake ya kwanza.

Baada ya kupadirishwa aliambiwa na wakuu wake kurudi Chuo Kikuu apate kuelimishwa zaidi. Basi, akapata shahada ya teolojia, akawekwa kusimamia parokia, na ndipo alipoanza maisha ya kujitoa na kujishusha kabisa kwa ajili ya wengine.

Watu wa parokia yake hawakuweza kuishi maisha adili; dhambi kubwa na maovu mengine yalienea sana. Lakini paroko wao alilisimamia kundi lake kama mchungaji mwema. Kwa sala, kufunga na upole wake aliwarudisha wakosefu wengi. Hivyo parokia ambayo kwanza ilikuwa mbaya, ikawa nzuri sana. Ile namna yake ya kuwafundisha siku za jumapili ilikuwa ya pekee. Aliwafanya wanafunzi watatu au wanne wajadiliane juu ya fadhila zilizokuwa kinyume cha kawaida mbaya za watu. Namna hiyo iliwavutia sana wanaparokia na kuwasaidia sana.

Zaidi ya hayo, alijitahidi kuistawisha hali yao ya kiuchumi kwa njia ya kuanzisha mfuko wa jumuiya; watu walitia hela walipofanikiwa katika biashara yao, na biashara ilipopungua walisaidiwa. Mradi huo ulikuwa mzuri sana kwa sababu kwa njia hiyo biashara iliendelea kukua na watu wengi zaidi walipewa kazi ya mshahara.

Kwa sababu ya hamu yake ya kuwapa watoto nafasi ya kufundishwa kusoma na kuandika, hata wale walioshindwa kulipa karo ya shule, aliwaitia wanawake wanne. Hao wakajitoa kabisa na baada ya muda usio mrefu shule ilifunguliwa isiyokuwa na karo yoyote. Baadaye wanawake wengine walijiunga na hao wanne wa kwanza, na hivyo kundi lao likawa shirika la masista wa Bikira Maria.

Wakati ule katika nchi nyingi za Ulaya uhusiano kati ya wakatoliki na waprotestanti ulikuwa mbaya sana, lakini padre Petro Furiye hakutaka iwe hivyo. Badala yake alitoa mfano wa upole na adabu katika kushirikiana nao. Alisisitiza kabisa kwamba ubaguzi wowote ule miongoni mwa Watoto ungepaswa kuwa mwiko; watoto waprotestanti wangekuwa hawana budi kutendewa kwa upendo na wema, wala neno lolote dhidi yao lisingetajwa.

Mwaka 1622, padre Petro alipokuwa na umri aa miaka hamsini na saba, aliitwa na askofu wa jimbo lake, naye akampa kazi ngumu: alirekebisha shirika lake la kitawa kwa kuirudishia nidhamu maana yake iliyo halisi. Hiyo ilikiwa kazi ngumu sana, hasa kwa kuwa watawa wenzake hawakumpokea kwa wema, wala kumkaribisha. Lakini mbele ya kazi hii ngumu iliyomkabili padre Petro hakukata tamaa wala hakulalamika. Kama vile zamani alivyojitoa kuibadili roho ya parokia yake ngumu, hivyo ndivyo sasa alivyojitoa kwa ajili ya shirika lake. Miaka kama saba hivi badaye, utii na nidhamu vilikuwa vikiwaongoza tena watawa wenzake wote. Na miaka mitatu kisha hapo, jambo gumu kuliko yote lilimwangukia: alichaguliwa kuwa padre mkuu wa shirika zima. Aliwaambia wajumbe waliomchagua kwamba, "Leo ninajitoa kwenu kwa wokovu wa roho zenu, wala si kwa ajili ya heshima au faida yoyote ile iwezayo kunipata".

Alifariki dunia mwaka 1640, 9 Desemba, baada ya kujitoa kwa uhodari kwa muda wa miaka arobaini, akipata nguvu yake kutoka kwa kanuni yake ya binafsi isemayo: "Kumsaidia kila mmoja, kutomdhuru yoyote". Kanuni hiyo yaweza kustawisha matendo mengi ya upendo maishani mwa kila mkristu. Padre Furiye alitangazwa Mtakatifu mnamo mwaka 1897

Maoni


Ingia utoe maoni